KLABU ya Mtibwa Sugar imesema imekwenda kwenye Ligi ya Championship kwa ajili ya kutalii lengo lao ni kujifunza na kupambana kurudi Ligi Kuu na somo kwa klabu nyingine.
Mtibwa Sugar ilishuka daraja msimu uliopita na mwaka huu inashiriki Ligi ya Championship kujaribu bahati yao ya kurejea kunako Ligi Kuu.
Akizungumza na Daily News Digital leo Msemaji wa Mtibwa Sugar Thobias Kifaru amesema kushuka kwao na kucheza Ligi hiyo ni kama wamekwenda kufanya utalii ili hatimaye wapambane na kurejea tena wanakostahili.
“Huku tumekuja kutembea naamini tutajifunza changamoto zilizopo ili hapo baadaye tukipanda turudi na somo la kuzipa klabu zilizoko juu ndio maana nasema tumekuja kutalii,”amesema.
SOMA: Mtibwa yaachana na Mayanga
Amesema anajua ligi hiyo ni ngumu kwa sababu kuna timu nyingi ziliwahi kushuka na kupotea kabisa lakini Mtibwa imejipanga vizuri isije ikapotea kama nyingine.
Mtibwa tayari imeanza kampeni ya kupanda Ligi Kuu vizuri baada ya mchezo wa kwanza na kushinda dhidi ya Green Warriors mabao 2-0 kwenye Uwanja wa Manungu, Turiani.
Itacheza dhidi ya Cosmopolitan Septemba 27 kwenye Uwanja wa Jamhuri Morogoro. Katika mchezo uliopita Cosmopolitan imetoka sare ya bao 1-1 dhidi ya African Sports.