Kihongosi aagiza anayedaiwa kumtorosha mwanafunzi asakwe

KATIBU wa Itikadi Uenezi na Mafunzo wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Taifa, Kenani Kihongosi amemuagiza Mkuu wa Wilaya ya Mkalama, Mosses Machali kumtafuta mtuhumiwa anayedaiwa kumtorosha mwanafunzi wa kidato cha kwanza katika Shule ya Sekondari Tumuli na atakapopatikana afikishwe kwenye mikono ya sheria.

Kihongosi alitoa agizo hilo wakati akisikiliza kero za wananchi katika mkutano wa hadhara uliofanyika Soko la Misigiri Iramba juzi. Kihongosi alichukua hatua hiyo baada ya mama aliyefahamika kwa jina la Vivian Stephano kulalamikia changamoto yake ya kupotelewa na mtoto wake aliyetoroshwa akiwa shule ya bweni na kufanya jitihada za kumtafuta bila mafanikio.

“Nikuagize mkuu wa wilaya utoke na huyu mama ukathibitishe kama huyo mtu yupo (baba aliyemuwekea dhamana) na kama yupo nitaomba kwa hatua zako atafutwe huyo mtu apatikane kama ni Geita gari iwashwe usiku huu (juzi) iende Geita na kama ni baba mzazi ina maana atakuwa anajua kijana wake yupo wapi. “Haki ya huyu mama ipatikane kwa sababu hata mimi naamini binti yupo na kwa kuwa alikuwa mwanafunzi mumfikishe kwenye vyombo vya sheria iwe funzo kwa wenye tamaa kama hizi,” aliagiza.

Kihongosi amesema ni muhimu kusimamia haki za wananchi, akionya kuwa kwa sasa siasa zimekuwa nyingi kuliko kujali utu wa watu, akimwelekeza mkuu wa wilaya kuhakikisha mama huyo hatumii gharama zake tena kumtafuta binti huyo. SOMA: Polisi yaomba ukatili wa kijinsia kuwa somo shuleni

Kadhalika, Kihongozi amewataka wazazi na walezi kuwalea watoto katika maadili mema ili wasishawishiwe kufanya vitendo visivyofaa. Machali alisema ofisi yake inatambua sakata la mama huyo na imeshachukua hatua ikiwemo kuzungumza na mkuu wa upelelezi wa wilaya. “Nilifuatilia mahudhurio ya yule binti huko nyuma na nilijiridhisha kuwa alikuwa mhudhuriaji mzuri shuleni hakuwa mtoro, niliwataka jeshi la polisi kuhakikisha mtuhumiwa aliyepatiwa dhamana anapatikana,” alisema.

Machali amesema mpaka sasa polisi imefanikiwa kumkamata aliyemwekea dhamana mtuhumiwa ambaye ni baba mzazi wa kijana anayedaiwa kumtorosha binti huyo na hatua inayofuata ni baba huyo kuwapeleka Katoro Geita alipo binti huyo. Pia, Machali amesema  wanaendelea kuchunguza maofisa wa polisi waliofanya uzembe na kusababisha mtuhumiwa kuachiwa kabla binti hajapatikana ili hatua zichukuliwe.

Vivian amedai alipewa taarifa na uongozi wa shule aende kumchukua mtoto wake shuleni lakini baada ya kufika shuleni hapo hakumkuta na baadaye kuambiwa akatoe taarifa polisi kwa sababu mwanae ametoroka na mwanafunzi wa kidato cha tatu aliyefahamika kwa jina la Edina (18). Amedai alitoa taarifa polisi na kupewa hati ya ukamataji ‘RB’ ya kumtafuta mwanae na baada ya kumtafuta kwa muda mrefu bila mafanikio alipata taarifa kuwa yupo mkoani Geita ambapo alienda Geita lakini hakumkuta.

Vivian amesema baadaye aliambiwa mtoto wake yupo Mwanza na alipoenda Mwanza alitoa taarifa kituo cha polisi Mabatini na kupewa usaidizi wa polisi na kwenda kumtafuta lakini hawakumpata na baadaye walirudi Geita na kwa maelekezo ya Edina aliwapeleka kwenye nyumba ya kijana anayetuhumiwa kuishi na wanafunzi hao kwa pamoja.

Amesema walifanikiwa kumkamata kijana aliyekuwa anaishi nao na kurudi nae Singida, aliwekwa mahabusu kwa siku nne lakini mtuhumiwa huyo alitolewa kwa dhamana aliyowekewa na baba yake mzazi kwa madai kama atapelekwa mahakamani Vivian hawezi kumpata mtoto wake. Amesema baada ya mtuhumiwa huyo kutolewa kwa dhamana alitoroka na Edina pia alitoroka, alipofuatilia aliambiwa polisi imemkamata mdhamini wake.

Mama huyo amedai alienda kuomba msaada kwa mkuu wa wilaya na alimsaidia kumfikisha kamanda wa polisi wa wilaya lakini aliamua kwenda kwa Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Singida lakini alipoeleza shida yake aliambiwa kamanda hayupo na kuelekezwa kwa msaidizi wa kamanda wa polisi mkoa hakumpa ushirikiano na kumfukuza.

Habari Zifananazo

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Back to top button