Kikwete amsifu Samia kwa maono

RAIS wa Serikali ya Awamu ya Nne, Jakaya Kikwete amesifu uamuzi wa Rais Samia Suluhu Hassan wa kuandaa Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050 sambamba na mpango wa utekelezwaji wake.

Kikwete alisema hayo Dodoma jana alipozungumza kwa niaba ya viongozi wastaafu wakati wa uzinduzi wa dira hiyo.

Alisema hatua hiyo ni muhimu kwani itarahisisha malengo yaliyomo kwenye dira kutekelezwa.

“Mimi nilipozindua dira ya mwaka 2000-2025 ilikuwa tufanye tathmini tuko wapi na tunakwenda wapi, baada ya tathmini mapendekezo yaliyowekwa ilikuwa tutengeneze mpango wa muda mrefu wa miaka 15, tukaugawa kwa miaka mitano mitano ambayo sasa ndiyo inakamilika… ndiyo maana tunatoa pongezi maalumu kwamba mpango huu toka mwanzo unatengenezewa utekelezaji wake,” alisema Kikwete.

Alisema anampongeza Rais Samia kwa uamuzi wa kutaka Tanzania iwe na Dira ya Taifa ya Maendeleo ya miaka 25 kutoka mwaka 2025-2050.

Kikwete alisema uamuzi huo umewathibitishia viongozi wastaafu na Watanzania na ulimwenguni kwa ujumla kuwa yeye (Rais Samia) ni kiongozi makini mwenye maono ya mbali na mapenzi makubwa kwa nchi yake.

“Wewe ni kiongozi mwenye dhamira ya dhati ya kuona nchi yetu na watu wake tunatoka hapa tulipo na tunakwenda kwenye hatua ya juu zaidi ya maendeleo kwa uhakika na utaratibu unaoeleweka na ulio wazi… tunakupongeza kwa jinsi mchakato wa kutayarisha dira ulivyoendeshwa, ulifanyika kwa weledi wa hali ya juu, ulikuwa shirikishi na jumuishi kwelikweli hata sisi wastaafu tulishiriki kutoa maoni yetu kama walivyoshiriki Watanzania wenzetu kutoa maoni yao,” alisema.

Kikwete alisema Dira ya 2050 inaakisi mahitaji, matarajio, matamanio na maoni ya Watanzania walio wengi na yeye alitoa maoni kadhaa lakini kubwa la msingi alieleza furaha yake ya kuona shabaha ya dira ni kuitoa Tanzania kutoka nchi ya uchumi wa kati ngazi ya chini na kufikia uchumi wa kati ngazi ya juu ifikapo 2050.

“Kama ambavyo dira ya 2000-2025 ya Rais Benjamin Mkapa ilitutoa kwenye kundi la nchi masikini sana duniani na kutufikisha hapa tulipo kwenye uchumi wa kati, ni matumaini yetu Watanzania wote na sisi wastaafu Dira ya 2050 ambayo mimi naiita ya Rais Samia itatufikisha kwenye nchi za uchumi wa kati daraja la juu kwa vigezo vinavyotambulika kimataifa.

“Hili ni jambo linalowezekana kama wapo wenzetu wameweza na sisi tunaweza, kama wao wameweza kwa nini sisi tusiweze, tunacho kila kitu cha kutuwezesha kufika huko na tukifika hapo itakuwa imetuweka hatua nzuri ya kufukuzia kuingia kwenye lile kundi la juu kabisa,” alisema.

Kikwete alisema jambo lingine analompongeza Rais Samia ni kuifikisha dira hiyo bungeni kwa wawakilishi wa wananchi: “Imepitishwa, imekubalika, utaratibu mzuri na mambo yanakwenda vizuri sana kitendo kinachojenga uhifadhi na utekelevu… kwa mambo yalivyofanyika sisi wastaafu tunasema hongera sana, umefanya jambo kubwa kwa historia na maendeleo ya nchi yetu, jambo ambalo litafanya jina lako liendelee kutajwa kila mwaka kwa miaka 25 mpaka mwaka 2050 na hata baada ya hapo”.

Aliongeza: “Nawaomba wananchi wenzetu wote tuisome dira tuielewe na tushirikiane na serikali, kuitekeleza, tunakutakia kila la kheri (Rais Samia) na ushindi mkubwa katika uchaguzi wa 2025”.

Habari Zifananazo

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Back to top button