Mradi bil 5/- kuing’arisha Lundamatwe

IRINGA: Diwani wa Kata ya Ilole, Erick Kikoti ameendelea kuimarisha mawasiliano kati ya viongozi na wananchi kupitia ziara ya kijiji kwa kijiji inayolenga kusikiliza na kutatua changamoto za wananchi katika vijiji sita vya kata hiyo.

Katika mkutano mkubwa wa hadhara uliofanyika Kijiji cha Lundamatwe na kuhudhuriwa na wananchi kutoka maeneo mbalimbali, Kikoti alisema dhamira yake ni kuhakikisha wananchi wanapata huduma bora na maendeleo ya kweli.

Akizungumza kwenye mkutano huo, aliwataka watumishi wa umma kuwajibika ipasavyo kwa wananchi baada ya kuwepo kwa malalamiko mengi kuhusu huduma katika zahanati ya kijiji.

Kutokana na malalamiko hayo, baadhi ya watumishi wa afya waliomba radhi mbele ya wananchi na kuahidi kuboresha utoaji wa huduma.

Diwani huyo pia aliwataka wenyeviti wa vitongoji kuimarisha ulinzi na usalama kufuatia kuongezeka kwa matukio ya wizi katika baadhi ya maeneo ya kata hiyo.

Katika hatua nyingine, Kikoti aliwaeleza wananchi kuhusu utekelezaji wa miradi mbalimbali ya maendeleo inayolenga kuinua uchumi wa Kata ya Ilole.

Miongoni mwa miradi hiyo ni ujenzi wa eneo kubwa la maegesho ya malori katika eneo la Mashamba ya Mkoa utakaogharimu zaidi ya Sh Bilioni 5.9.

Alisema mradi huo utahusisha maegesho ya malori zaidi ya 80, kituo cha mafuta, maduka pamoja na hoteli kwa ajili ya wageni na wafanyabiashara.

Kwa mujibu wa Kikoti, Serikali Kuu inatarajiwa kutoa zaidi ya Bilioni 5 na Halmashauri kuchangia Milioni 900 kupitia mapato ya ndani.

Alieleza kuwa mradi huo ambao tayari umepokea Sh Milioni 500 kutoka serikali kuu unatarajiwa kuongeza ajira, kukuza biashara ndogo na kubwa pamoja na kuongeza mzunguko wa fedha katika kijiji na maeneo jirani.

Mbali na mradi huo, alisema Serikali inaendelea na mipango ya kuboresha huduma za maji na umeme ambapo mradi wa maji wa zaidi ya Milioni 200 unatarajiwa kuanza Kibati huku maandalizi ya usambazaji umeme Mjimwema yakiwa yamekamilika.

Kikoti aliwahimiza wananchi kushiriki kulinda miradi hiyo na kushirikiana na viongozi ili kuhakikisha maendeleo yanapatikana kwa manufaa ya kizazi cha sasa na kijacho.

Ziara hiyo itaendelea katika vijiji vingine vya Kata ya Ilole huku mkutano mkubwa mwingine ukitarajiwa kufanyika hivikaribuni katika kijiji cha Kitelewasi.

Habari Zifananazo

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Back to top button