Kim amrudisha Kakolanya Stars

Kipa wa Klabu ya Simba Beno Kakolanya

KOCHA Mkuu wa Taifa Stars, Kim Poulsen baada ya miaka mitatu jana alimjumuisha kipa namba mbili wa Simba, Beno Kakolanya kwenye kikosi cha Taifa Stars kinachojiandaa na mchezo wa kufuzu fainali za Kombe la Mataifa ya Afrika kwa wachezaji wa ndani (Chan).

Kim Poulsen, kocha mkuu wa timu ya taifa, Taifa Stars

Kakolanya mechi ya mwisho ilikuwa 2019, Stars ilipocheza dhidi ya Burundi katika mchezo huo alidaka Juma Kaseja na Tanzania ilifungwa kwa mikwaju ya penalti. Kikosi cha Stars kinajiandaa na mchezo dhidi ya Uganda, ambao utapigwa Agosti 28 nchini Uganda kabla timu hizo kurudiana Septemba 3, Dar es Salaam.

Kim alisema kikosi cha wachezaji 25 kitaingia kambini kesho Jumapili Agosti 21, kujiandaa na mchezo dhidi ya Uganda. Alisema wachezaji aliowaita ni wale walikuwepo awali na baadhi ya nyota ambao wamewaongezea katika kuimarisha kikosi kuelekea katika mchezo huo.

Advertisement

Wachezaji 25 aliowaita ni Aishi Manula, Abutwalib Mshery, Kakolanya, Kibwana Shomari, Mohammed Hussein, Paschal Msindo, Nathan Chilambo, Dickson Job, Bakari Mwamnyeto, Kennedy Juma, Sospeter Bajana na Jonas Mkude. Wengine ni Mzamiru Yassin, Kelvin Nashon, Feisal Salum, Farid Mussa, Abdul Seleman, Relliants Lusajo, Kibu Denis, Habib Kyombo, George Mpole, Anwar Jabir, Danny Lyanga na Salum Abubakar.