Kipa Simba Queens nje ya uwanja msimu mzima

KLABU ya Simba Queens itakosa huduma ya golikipa wake Coraline Rufa atakayekuwa nje ya uwanja kwa msimu mzima baada ya kufanyiwa upasuaji wa goti.
 
Rufa raia wa Kenya alipata majeraha hayo katika mchezo wa nusu fainali kufuzu Ligi ya Mabingwa Afrika kwa wanawake ukanda wa CECAFA dhidi ya Kenya Police Bullets uliofanyika Ethiopia, Agosti 2024.
Daktari wa Simba, Naima Mohammed amesema upasuaji huo unasababisha kipa huyo kukaa nje ya uwanja kwa miezi nane kabla ya kurejea dimbani ambapo atakosa msimu huu wote wa Ligi Kuu ya Wanawake Tanzania Bara.
 
“Upasuaji umeenda vizuri na matarajio yetu ni kwamba baada ya kupona atakuwa tayari kurudi uwanjani kuendelea na majukumu yake ya kutumikia klabu ya Simba kwa msimu mwingine,” amesema Naima.