KITUO cha afya Sumbawanga Asilia kilichopo Manispaa ya Sumbawanga mkoani Rukwa kinatarajiwa kuhudumia wananchi zaidi ya 50,000 wa kata za jirani za Momoka na Mafulala.
Waziri wa Maliasili na Utalii, Balozi Pindi Chana ametoa taarifa hiyo leo Oktoba 2, mara baada ya kuweka jiwe la msingi katika kituo hicho.
Chana amesema kituo hicho kimetumia takribani Sh milioni 250, kukamilika kwake kutarahisisha upatikanaji wa huduma ya afya.
SOMA: Majaliwa ataka uchunguzi miradi ya afya Rukwa
Amemuelekeza mkandarasi anayejenga kituo hicho kukikamilisha kazi kwa wakati ili wananchi wapate huduma bora. Aidha, amewataka wananchi kukitunza na kukitumia vizuri kituo hicho kwa manufaa ya afya zao.
Naye, Kaimu Mganga Mkuu, Dk Louis Massawe amesema kwa sasa mradi uko katika hatua za mwisho za ukamilishaji ikiwemo uwekaji wa vigae pamoja na vioo.
Amesema mradi huo unajumuisha ujenzi wa jengo la wagonjwa wa nje (OPD), maabara na choo cha nje hadi kufikia sasa jumla ya Sh milioni 163.8 zimeshatumika.