Kituo cha kupozea umeme Nyakanazi kupanuliwa

GEITA: SERIKALI kupitia Wizara ya Nishati imepanga kufanya upanuzi wa kituo cha kupoza umeme Nyakanazi kilichopo wilayani Biharamulo ili kuunganisha mfumo wa gridi ya taifa na kutanua uwigo wa huduma ya umeme.
Mpango huo unalenga kutengeneze mfumo ambao utaunganisha gridi yote ya taifa ndani nchi ya Tanzania na kuunda mfumo mmoja uliounganishwa na kuliwezesha taifa kuuza umeme nje ya nchi.
Mhandisi Msimamizi wa Kituo cha Kupoza Umeme Nyakanazi, Mhandisi Isack Kisandu ametoa taarifa hiyo mbele ya waandishi wa habari mkoani Geita walipofanya ziara maalum kutembelea kituo hicho.
Amesema mpaka sasa kituo hicho kina njia kuu tatu ambazo zote zina uwezo wa Kilovati 220 ambapo upanuzi ukikamilika utaongeza kiwango cha umeme kwenye kila njia hadi kufikia Kilovati 400.

“Laini moja inapokea umeme kutoka Geita ambayo ina umeme wa gridi ya taifa, laini ya pili inapokea umeme kutoka kituoz cha kufua umeme cha Rusumo na laini ya tatu inapeleka umeme Kigoma.
“Tunataka kupanua kituo kwa ajili ya kuunganisha gridi nzima ya taifa kwani kuna maeneo mengine kama Sumbawanga ambao wanapata umeme kutokea nchini Zambia”, amesema Mhandisi Kisandu.
Amesema kituo kina mashine umba (transifoma) mbili zenye uwezo wa 40 MVA kila moja ambazo zinasaidia kupunguza kiwango cha voltage kutoka Kilovoti 220 kwenda 33 Kilovoti kwa ajili ya matumizi.

Amesema pia kituo cha Nyakanazi kina mashine vilishio (feeder) kuu nne ambazo zinalisha kwenye wilaya saba zilizopo kwenye mikoa mitatu tofauti nchini.
“Kwa mkoa wa Kagera tunalisha wilaya ya Ngara na Biharamulo, kwa mkoa wa Geita tunalisha wilaya ya Chato, Bukombe na Mbogwe huku kwa Kigoma kuna wilaya ya Kakonko na Kibondo.
“Tuna eneo kubwa sana la kupeleka umeme kwa ajili ya wananchi kwani kituo cha Nyakanazi ni kituo cha kwanza kinachpokea umeme kutoka kituo cha kufua umeme cha Rusumo”.
Amesema kituo cha Nyakanazi kinapokea wastani wa Megawati 27 kutoka Rusumo ambapo wilaya zinazopokea umeme kutoka hicho zinatumia takribani Megawati 19 na kusalia na ziada kwenye gridi.



