KOCHA wa zamani wa Liverpool, Jürgen Klopp ameteuliwa kuwa mkuu wa soka wa kampuni ya Rell Bull duniani.
Klopp mwenye mwenye umri wa miaka 57 ataanza jukumu hilo Januari 1, 2025.
Red Bull imesema Klopp hatashriki oparesheni za kila siku lakini atazishauri timu kuhusu falsafa za kucheza, mikakati ya uhamisho na maendeleo ukocha.
SOMA: Klopp kuachana na Liverpool mwishoni mwa msimu huu
“Miezi michache iliyopita nilisema sioni tena nafasi yangu kwenye benchi, na hali hiyo bado ipo. Lakini bado napenda soka, bado napenda kufanya kazi, na Red Bull inanipa jukwaa kamili kwa ajili ya hilo,” amesema Klopp kupitia mtandao wa Instagram.
Kampuni ya Red Bull inamiliki klabu za RB Leipzig inayoshiriki Bundesliga, Red Bull Salzburg ya Ligi Kuu Austria na New York Red Bulls ya Ligi Kuu Marekani pamoja na klabu ya Red Bull Bragantino iliyopo Brazil.
Afisa Mtendaji Mkuu wa kampuni hiyo anayeshughulika na uwekezaji na miradi Oliver Mintzlaff amesema: “Jürgen Klopp ni mmoja wa watu mashuhuri na wenye ushawishi mkubwa katika soka duniani, akiwa na ujuzi wa hali ya juu na mvuto wa kipekee.”
Klopp alishinda mataji nane katika kipindi cha miaka tisa Liverpool yakiwemo Ligi Kuu England, Ligi ya Mabingwa Ulaya kabla ya kuachia ngazi mwisho wa msimu uliopita.