Kocha Dodoma Jiji kujipanga upya

Kikosi cha Dodoma Jiji

BAADA ya kuanza Ligi Kuu Bara kwa kupoteza michezo miwili mfululizo nyumbani, Kocha Mkuu wa Dodoma Jiji Masoud Djuma amesema atayatumia mapumziko kuangalia madhaifu ya kikosi chake ili yasijirudie katika mchezo wa tatu.

Dodoma Jiji ilianza ligi kwa kichapo cha mabao 3-1 kutoka kwa Mbeya City kabla ya juzi kukubali kipigo cha mabao 2-1 kutoka kwa Tanzania Prisons. Akizungumza na gazeti hili, Djuma alisema k hafurahishwi na mwenendo alioanza nao msimu wa 2022/23 baada ya kushindwa kupata pointi kwenye michezo miwili hivyo atatumia mapumziko kujiuliza.

“Hakuna mwalimu anayefurahi kuona anashindwa kupata matokeo katika michezo mfululizo hivyo nimeyaona mapungufu ya kikosi changu naenda kuyafanyia kazi makosa yote yaliyojitokeza katika michezo iliyopita ili tuweze kurudi kivingine,” alisema Djuma.

Advertisement

Baada ya mechi za jana, ligi itasimama kwa takriban wiki tatu kupisha michuano ya kimataifa. Kwa upande wa kocha wa Prisons, Patrick Odhiambo, alisema anawapongeza wachezaji wake kwa ushindi walioupata kwani waliingia uwanjani wakijua kuwa wanaenda kukutana na timu bora hivyo wakajipanga vyema kuwakabili wapinzani wao ndio maana wamekusanya pointi tatu ugenini.

“Huu ulikuwa mchezo muhimu kwetu tulihitaji pointi tatu ili kurejesha hali ya kujiamini kikosini mwetu tumetoka kupoteza mchezo uliopita hivyo matokeo haya yanapunguza wigo presha kikosini na kuongeza morali yetu,” alisema Odhiambo.