Kocha wa viungo Simba aanza tambo
BAADA ya Simba kumtambulisha rasmi kocha wa viungo, Kelvin Mandla kutoka nchini Afrika Kusini, amejinasibu kuwa anatazamia wataifikisha mbali Simba katika mashindano ya kimataifa hatua ambayo hawajawahi kufika.
Akizungumza na gazeti hili baada ya kutambulishwa, Mandla ambaye amechukua nafasi ya Sbai Karim alisema anafuraha ya kuwa sehemu ya benchi la ufundi la Simba ambayo ni klabu kubwa Afrika.
“Simba ni timu kubwa Afrika, ni timu ambayo sio tu inashiriki bali kushindana kwenye michuano ya CAF.
Natazamia kuungana nao katika jambo hilo na kusaidia timu kwenda mbele zaidi ya ambapo imewahi kufika,” alisema Mandla.
Kutambulishwa wa kocha huyo kunatarajiwa mabadiliko makubwa katika utimamu wa miili ya wachezaji wa Simba, ambao wamekuwa wakilalamikiwa kushindwa kuhimili upinzani kutoka kwenye timu pinzani katika michezo ya Ligi Kuu Tanzania Bara msimu huu. Mandla mwenye umri wa miaka 30 amesaini mkataba wa mwaka mmoja na ana leseni B ya ukocha wa viungo kutoka Shirikisho la Soka Ulaya (Uefa) aliyoipata nchini Scotland.
Kabla ya kujiunga na Simba alikuwa Mkuu wa Kitengo cha Afya na Utimamu wa mwili wa timu ya Taifa ya Afrika Kusini ‘Bafana Bafana’ timu ya Taifa ya Wanawake ‘Banyana Banyana’, timu ya Taifa ya vijana chini ya umri wa miaka 17 na 20 tangu mwaka 2018 hadi sasa.
Pia amewahi kuwa Mkuu wa Kitengo cha upimaji wa afya za wachezaji, Mpumalanga Sports, kazi ya muda kuanzia mwaka 2021 hadi sasa. Mkuu wa Kitengo cha Sayansi ya Afya na Utimamu wa mwili wa timu ya wanawake; Chuo Kikuu cha Johannesburg (2019-2021).
Mkuu wa Kitengo cha Sayansi ya Afya na Utimamu wa mwili wa timu za kikapu, raga na kriketi: St. John College 2018, kocha msaidizi wa viungo wa timu ya wakubwa ya Orlando Pirates (2017- 2019).
Kocha msaidizi wa viungo wa timu ya akiba ya Kaizer Chiefs (2017 kazi ya muda miezi mitatu).