Kuuza makaa ya mawe ni fursa -Makalla

MASASI: CHAMA Cha Mapinduzi (CCM) kimesema kuwa makaa ya mawe ni fursa ya kiuchumi kwa kuongoza mapato kwa taifa na kwa viwanda nchini, hivyo kuuzwa kwa malighafi hiyo nje ya nchi si haramu.

Katibu wa Halmashauri Kuu (NEC), Itikadi, Uenezi na Mafunzo wa CCM, Amos Makalla ameeleza hayo leo Aprili 17,2025 wakati akizungumza na wananchi wa Wilaya ya Masasi mkoani Mtwara, ikiwa ziara yake ya siku kumi katika mikoa ya Lindi na Mtwara.

Makalla ameeleza hayo akijibu hoja ya Makamu Mwenyekiti wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), John Heche aliposema kuwa anapishana na maelfu ya magari yanasomba makaa ya mawe kutoka kusini na kuwaacha vijana wa nchi wanabaki na mashimo.

Makalla amesema kuwa mambo hayo yanahitaji ubobevu wa kuelewa kuhusu biashara na uchumi akifafanua kuwa si kila gari linalobeba makaa ya mawe yanapeleka nje ya nchi kwani malighafi hiyo inahitajika katika mambo mengi ikiwemo maendeleo ya viwanda nchini.

Pia amesema kuwa makaa ya mawe kuuzwa nje ya nchi sio biashara harama kwa sababu ni fursa nzuri inayosaidia serikali na taifa kwa ujumla kuongeza mapato na fedha za kigeni zinazosaidia kufanya maendeleo ya nchi kutokana na masoko yanayopatikana nje ya nchi.

“Kuwa na makaa ya mawe ni fursa kwa sababu yanatumika katika kazi mbalimbali na hapa ndani ya nchi uhitaji wa makaa ya mawe ni mkubwa katika kwenye viwanda vyetu,” amesema Makalla.

Ameongeza: “Kwahiyo namwambia John Heche mbali ya kupata fursa ya masoko nje ya nchi na kutuingizia fedha za kigeni ambazo tunazipata na tunapata kodi yetu na Rais anapata uwezo wa kujengo shule, kuweka miradi ya maji na kujenga barabara kwahiyo sisi makaa ya mawe ni fursa ya kupata fedha na kuuza nje sio haramu ni kuongeza mapato”.

Pia Makalla amesema kuwa Tanzania makaa ya mawe yanatoka kusini na kuna viwanda vya saruji nchini ambavyo vinahitaji uwepo wa makaa ya mawe kikiwemo kiwanda cha saruji cha Wazo, Tanga Cement na cha Dangote vyote vinauhitaji wa malighafi hiyo.

Habari Zifananazo

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Back to top button