DAR ES SALAAM: Waziri wa Viwanda na Biashara Dk. Ashatu Kijaji amesema lengo la Serikali ya Awamu ya Sita nikuona viwanda vya saruji nchini vinazalisha saruji kwa ubora na viwango vya kimataifa ili viweze kukidhi mahitaji na ushindani wa soko la ndani na nje ya nchi.
Amesema hayo katika Kikao cha wazalishaji wa saruji nchini kilichofanyika Jijini Dar es Salaam ikiwa ni muendelezo wa kukutana kila baada ya miezi mitatu ili kusikiliza na kutatua changamoto zinazowakabili ili kuongeza uzalishaji wa saruji wenye tija.
Aidha, Waziri Kijaji amewaahidi wazalishaji hao wa saruji kuwa Serikali inaendelea kutatua changamoto mbalimbali wanazokabiliana nazo ikiwemo miundombinu ya umeme, barabara na maji ili kuboresha uzalishaji wa viwanda vya saruji nchini.
Pia, Dk. Kijaji amewashauri wazalishaji hao kuzalisha saruji yenye ubora ili Saruji ya Tanzania iweze kuingia katika Soko la Eneo Huru la Biashara Afrika (AfCFTA) kutokana na ukubwa wa soko hilo lenye wateja zaidi ya bilion 1.3.
Kwa upande Mwingine, Dk. Kijaji amebainisha kuwa hadi sasa uzalishaji wa saruji nchini ni tani milioni 11 kwa mwaka, mahitaji ya ndani ni takriban tani milioni 7.5. na ziada huuzwa nje ya nchi.
Naye, Mwenyekiti wa Shirikisho la wenye Viwanda Tanzania (CTI), Leodga Tenga ameiomba serikali kuendelea kuboresha mazingira bora kwa wawekezaji na wafanyabiashara huku akiwashauri wamiliki hao wa viwanda kuzalisha saruji yenye ubora na wingi ili kuweza kushindana katika soko la ndani na nje.
Mkurugenzi wa Kiwanda cha Saruji Tanga Tanzania na Mjumbe wa Bodi ya CTI Mhandisi, Benedict Lema ameishukuru Serikali kwa kuendelea kutatua changamoto mbalimbali na amesema kwa niaba ya wamiliki wa viwanda hivyo wapo tayari kushirikiana na serikali katika kutatua changamoto mbali mbali ili kuweza kuboresha uzalishaji wa saruji nchini.