Ligi ya Mkoa Geita yalamba udhamini wa Kampuni ya madini

GEITA: KAMPUNI ya Hexad Company Limited ya mjini Geita inayojishughulisha na uchimbaji wa madini imeingia makubaliano na Shirikisho la Soka mkoani Geita (GEREFA) kwa ajili kudhamini Ligi ya soka ya Mkoa.

Mkurugenzi wa Kampuni ya Hexad, John Luhemeja amethibitisha hayo katika mkutano na waandishi wa habari na kueleza dhamira ni kusaidia maendeleo ya soka mkoani hapa.

Amesema udhamini huo unahusisha utoaji wa vifaa vya michezo pamoja na gharama za uendeshaji huku tathimini ya awali inaonyesha takribani Sh milioni sita itatumika kama gharama za awali.

“Tunatoa udhamini huu kwa shabaha ya kukuza vipaji vya vijana wetu, ili hapo mbeleni waweze kujiajiri, lakini kubwa lingine tutengeneze Geita Gold nyingine kutokana na hawa vijana.”

Luhemeja amesema udhamini huo umeanzia hatua ya robo fainali ya ligi ya Mkoa msimu huu ambapo timu zote nane zimepatiwa vifaa na udhamini huo unatarajiwa kuendelea kadri ya mahitaji.

Mwenyekiti wa Gerefa, Salum Kulunge amekiri udhamini huo utanufaisha timu zote zilizoingia hatua ya nane bora ya Ligi ya Mkoa na itasaidia ushiriki wa timu zote kufanikiwa kumudu gharama za ushiriki.

Kulunge amewaomba wadau wengine kujitokeza kuunga mkono udhamini huo ili Mkoa uendelee kupiga hatua zaidi kwenye maendeleo ya soka kwa kuongeza idadi ya timu zinazoshiriki ligi kuu Tanzania bara.

 

Habari Zifananazo

Back to top button