Liverpool yamfikiria Giorgi Mamardashvili

Golikipa wa Valencia, Giorgi Mamardashvili.
KLABU ya Liverpool inafikiria uhamisho wa golikipa wa Valencia Giorgi Mamardashvili kwa ada ya pauni milioni 35 huku kukiwa na uwezekano baadaye kupelekwa kwa mkopo.
Golikipa huyo wa kimataifa wa Georgia, 23, anaonekana kuwa uwekezaji wa muda mrefu lakini Liverpool haihitaji golikipa majira haya ya kiangazi labda Caoimhin Kelleher aondoke.
Mkataba wa Mamardashvili katika klabu hiyo ya Ligi Kuu ya Hispania- LaLiga unatarajiwa kumalizika mwaka 2027.
Golikipa wa Liverpool, Caoimhin Kelleher.
Mamardashvili aliyetoka kituo cha kukuza vipaji cha Dinamo Tbilisi alijiunga na Valencia moja kwa moja mwaka 2022 kufuatia kipindi cha mkopo katika timu hiyo na ameendelea kuwa chaguo namba moja la timu hiyo ya Hispania.
Pia alicheza mechi zote za Georgia wakati wa michuano ya Kombe la Ulaya-Euro 2024 akisaidia nchi yake kutinga hatua ya 16 bora, huku ikiifuta Ureno mabao 2-0 katika mchezo wa mwisho wa makundi.
Liverpool ilimtumua Kelleher kwa kipindi kirefu cha msimu wa 2023-24 baada ya golikipa namba moja Alisson kupata majeraha ya nyama za paja.