Maandalizi Maonesho ya 47 ya Sabasaba yaanza

MAANDALIZI ya Maonesho ya 47 ya Biashara ya Kimataifa ya Dar es Salaam maarufu kama Sabasaba yameanza kwani hadi sasa nchi 14 zimethibitisha kushiriki zikiwemo kampuni 112 kutoka nje ya nchi na 1,188 za ndani ya nchi.

Kaimu Mkurugenzi wa Idara ya Ukuzaji Biashara TantradE, Fortunately Mhambe alisema hayo katika taarifa yake aliyoitoa kwa vyombo vya habari juzi kuhusu maandalizi hayo.

Alitaja baadhi ya nchi hizo kuwa ni China, Falme za Kiarabu, Uturuki, Kenya, Ghana, India, Singapore na nyinginezo.

Alisema kwenye maonesho hayo, Tantrade imeboresha maeneo mbalimbali ikiwa ni pamoja na kuweka programu za kuvutia kwa lengo la kuwakutanisha wafanyabiashara wa ndani na nje ya nchi, kuwapa fursa ya kutangaza bidhaa na huduma zao ikiwa ni pamoja na kutafuta masoko.

“Kaulimbiu ya maonesho haya ni “Tanzania mahali sahihi pa biashara na uwekezaji,” alisema.

Katika hatua nyingine alisema programu mojawapo ya maonesho hayo inajulikana kama ‘Sabasaba Expo Village’ ambayo inatangaza fursa zilizopo katika sekta ya madini, teknolojia ya habari na mawasiliano, gesi na mafuta.

Alisema Sabasaba Expo Village ni jukwaa muhimu ambalo linawezesha wafanyabiashara kushiriki, kuonesha bidhaa zao na kutafuta masoko.

“Eneo hili linatoa fursa kwa wafanyabiashara wa ndani na nje ya nchi kuonyesha ubunifu wao na kushirikiana na wadau wengine katika sekta mbalimbali.

“Kupitia Sabasaba Expo Village tunatarajia kuona ukuaji wa biashara, kuongezeka kwa mtazamo na kuimarisha uchumi wa nchi,” alisema.

Aliwataka wafanyabiashara kushiriki katika maonesho hayo kwa kuwa ni nafasi nzuri ya kukuza biashara zao, kujenga mtandao wa kibiashara na kuimarisha mchango wao katika maendeleo ya nchi.

 

Habari Zifananazo

Back to top button