Mabilioni ya China kusaidia kutokomeza umaskini

Waziri wa Fedha na Mipango, Dk. Mwigulu Nchemba, akionesha hati ya makubaliano yaliyofikiwa katika Mkutano wa 6 wa Kamati ya Pamoja ya Uchumi, Ufundi na Biashara kati ya Tanzania na Jamhuri ya Watu wa China. Uliofanyika kwa njia ya Mtandao Jijini Dar es Salaam. Kushoto ni Kamishna Msaidizi wa Idara ya Fedha za Nje Bw. Melkizedeck Mbise, kutoka Wizara ya Fedha na Mipango.

WAZIRI wa Fedha na Mipango, Dk Mwigulu Nchemba, amesema serikali inatarajia kunufaika na mpango wa msaada wa miaka mitatu utakaogharimu dola za Marekani bilioni 30, ulioahidiwa na Rais wa China, Xi Jinping wa kuzisaidia nchi za Afrika kukabiliana na umaskini.

Dk Nchemba alitoa kauli hiyo jijini Dar es Salaam alipozungumza kwa njia ya mtandao na Naibu Waziri wa Biashara wa China, Qian Keming, wakati wa mkutano wa sita wa Kamati ya Pamoja ya Uchumi, Ufundi na Biashara kati ya Tanzania na China.

Alisema msaada huo ulioahidiwa na Rais Jinping, Novemba, mwaka jana, Mjini Dakar, Senegal, kupitia mpango wa ushirikiano wa China na Afrika wa mwaka 2035, utasaidia upatikanaji wa fedha kwa ajili ya utekelezaji wa miradi ya maendeleo hapa nchini.

Advertisement

Alisema kupitia mpango huo, miradi tisa imekusudiwa kutekelezwa katika sekta za afya, kilimo, kutokomeza umasikini, kuendeleza biashara, uwekezaji, ubunifu wa teknolojia, kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi, kujenga uwezo na uhusiano wa moja kwa moja wa watu wa nchi hizo mbili.

Aidha, aliishukuru China kwa misaada iliyochangia kufanikisha miradi mbalimbali nchini ikiwemo miundombinu ya reli, elimu, Tehama, nishati, maji, kilimo, maendeleo ya viwanda pamoja na afya na kwamba misaada hiyo itaendelea kutolewa ili kuiwezesha nchi kukabiliana na umaskini na kukuza uchumi wake.

Kwa upande wake, Naibu Waziri Keming, aliahidi kuwa nchi yake itaendeleza uhusiano na ushirikiano na Tanzania kiuchumi na kijamii ili kutimiza malengo yake ya kupiga hatua kimaendeleo na kuboresha maisha ya watu wake.

Mkutano huo umewashirikisha mawaziri kadhaa wa Kisekta Pamoja na Waziri wa Fedha na Mipango wa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar, Dk Saada Salum Mkuya, Katibu Mkuu Wizara ya Fedha na Mipango, Emmanuel Tutuba na maofisa kadhaa kutoka Wizara ya Fedha na Mipango pamoja na Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki.

Add a comment

Toa Jibu

Barua-pepe haitachapishwa. Fildi za lazima zimetiwa alama ya *