KATIKA kipindi cha miezi mitano cha kuanzia Julai mwaka huu hadi Desemba Mosi mwaka huu, Wizara ya Madini imefanikiwa kukusanya zaidi ya Sh bilioni 434 katika maduhuli yake yote yaliyopo kote nchini na huenda wakavuka malengo ya Sh trilioni 1 hadi June 2025.
Waziri wa Madini, Antony Mavunde amesema hayo jana muda mfupi kabla ya kuzindua mnada wa uuzwaji wa madini ya vito yaliyofanyika ndani ya ukuta wa Magufuli Mirerani wilayani Simanjiro Manyara.
Mavunde alisema katika kipindi cha mwaka wa fedha 2024/25 malengo ya wizara ni kukusanya zaidi ya shilingi Trilioni moja na huenda malengo hayo yakavukwa kwani hadi kufikia Desemba 31 mwaka huu wamepanga kukusanya Sh bilioni 500.
Alisema Wizara ya Madini ni Wizara nyeti na serikali inategemea katika kuendesha uchumi wa nchi na makusanya katika Wizara hiyo yamekuwa yakiongezeka mwaka hadi mwaka kwani katika kipindi cha mwaka 2015/16 Wizara ya Madini ilifanikiwa kukusanya Sh bilioni 161
Waziri Mavunde alisema katika mwaka wa fedha 2023/24 Wizara ya Madini ilikusanya zaidi ya Sh bilioni 753 kutoka katika vyanzo vyake mbalimbali vya maduhuli na kuonyesha wazi kuwa sekta hiyo ikisimamiwa vizuri na watendaji kufanya shughuli zao kwa uadilifu na uaminifu sekta hiyo ni moja ya muhimili mkubwa wa serikali katika kuongeza mapato.
Alisema katika kuboresha sekta hiyo ya madini katika kitengo cha makusanyo Wizara ya Madini imejipanga kikamilifu ikiwa ni pamoja na kurudisha minada na maonyesha ya madini ya vito ya kitaifa na kimataifa ili wafanyabiashara wakubwa kwa wadogo wa ndani na nje waweze kunufaika katika minada hiyo na serikali iweze kupata mapato.
Waziri Mavunde alisema urejeshaji wa minada ya vito nchini ni jitihada za serikali kutaka ushirikishwaji kwa wachimbaji na serikali ili kufanya shughuli za uchimbaji na biashara ya sekta ya madini kwa uwazi na kufuata sheria na kanuni zilizowekwa.
Alisema minada yote itakuwa ikifanywa kwa njia ya kieletroniki ikiwa ni pamoja na kufanyika kwa njia ya uwazi na uwepo ya minada hiyo ni chachu ya maendeleo kote nchini hivyo aliwaondoa shaka wachimbaji kuwa hakuna atayeporwa madini yake na serikali.
”Minada yote itafanywa kwa njia ya kielekronic lengo ni kutaka kuona kila kitu kinafanywa kwa uwazi na ukweli na wenye kununuwa madini ya vito wanunuwe kwa njia ya haki bila ya kuwa na upendeleo wowote,”alisema Mavunde
Akizungumzia mnada wa madini ya vito ya Mirerani ambayo mengi yalikuwa Madini ya Tanzanite ,Waziri Mvunde alisema thamani ya madini yaliyouzwa jana ni zaidi ya Sh bilioni 3 yenye uzito wa gramu 1284.60 na amewashukuru wafanyabiashara wa madini wakubwa kwa wadogo kwa kujitokeza katika mnada huo.
Waziri Mvunde alisema kuwa serikali iko katika mkakati madhubuti ya kurejesha hadhi ya madini ya viyo ya Tanzanite ili jiwe hilo liwe na thamani kubwa nyakati zote kitaifa na kimataifa hivyo aliwataka wafanyabiashara wa sekta hiyo kushirikiana na serikali katika kufanikisha hilo.
Naye Makamu Mwenyekiti wa Kamati ya Bunge ya Nishati na Madini, Kirumbe Nyenda alimpongeza Waziri wa Madini kwa kuwa na ushirikiano wa kutosha na kamati hiyo na kuifanya Wizara hiyo kuendelea kupaa katika ukusanyaji mapato ya serikali.
Nyenda alisema pamoja na hayo pia alimshukuru Mavunde kwa kutatua baadhi ya changamoto zinazoikabili sekta hiyo kwa wachimbaji wakuwa kwa wadogo na kuonyesha wazi kuwa biashara katika sekta hiyo inafanywa kwa kufuata sheria.
”Tunaiomba Wizara ya Madini iendelee kujipanga kikamilifu katika kuiongozea mapato serikali na kutatua changamoto zote za wachimbaji nchini ili shughuli za uchimbaji na biashara zifanywe kwa umakini wenye kufuata sheria zilizowekwa”alisema
Naye Mkuu wa Mkoa wa Manyara,Qunne Sendiga mbali ya kumshukuru kurudisha minada kote nchini hususani katika Mji wa Mirerani pia alimwomba Waziri Mvunde kuhakikisha anasimamia umaliziaji wa jengo la soko la madini lililopo Mirerani.
Alisema jengo la Tanzanite Tower lililojengwa katika Mji wa Mirerani linagharimu kiasi cha shilingi Bilioni 5.4 na Mkandarasi ametishia kujitoa kwani amekuwa hali