Madiwani wahoji wachezaji Geita Gold kutolipwa

MADIWANI wa Halmashauri wa Mji wa Geita wameiomba ofisi ya Mkurugenzi wa Halmashauri hiyo kuweka wazi mapato na matumizi ya timu ya Geita Gold ili kujibu fununu za baadhi ya wachezaji kutolipwa mishahara.

Hoja hiyo imeibuliwa na diwani wa viti maalumu, Farida Mfuruki katika kikao cha baraza la madiwani na kuhoji mwenendo wa timu ili kupata uhalisia na utatuzi wa changamoto zinazoripotiwa ndani ta timu.

Makamu Mwenyekiti wa Halmashauri ya Mji wa Geita, alihoji juu ya taarifa za migomo ya wachezaji inayodaiwa kuwepo kwa kucheleweshewa stahiki zao na kuwataka wasimamizi kutoa ufumbuzi.

“Timu ni ya wananchi, wana haki ya kujua kinachoendelea na pengine huko mbele wakiona haiwafai kwa kuwa ni timu yao wanaweza wakaamua vinginevyo, hivo wanapaswa kujua maendeleo ya timu yao.”

Makamu Mkurugenzi wa Halmashauri ya Mji wa Geita, Egidy Teulas amekanusha uwepo wa changamoto ya malipo kwa wachezaji na kueleza kuna usimamizi tabiti wa mradi wa timu na hakuna tatizo.

“Sisi hatudaiwi chochote na kiuhalisia tumeshalipa, waliokuwa wanadai ni wachache waliokuwa na utovu wa nidhamu ambao walikatwa kwenye mishahara.” Anafafanua.

Anaongeza “Hata huyu Bwana George Mpole hakulipwa mshahara wa mwezi mmoja, lakini tunashangaa akaanza kutafutwa anasema viongozi hawajui alipo, siyo sahihi tulikuwa tunajua alipo.”

Taarifa ya Katibu Msaidizi wa Timu ya Geita Gold, Ramadhan Bukambu anasema kwa robo ya kwanza ya mwaka wa fedha 2022/23 na hadi Julai mosi, 2022 mapato ya timu ilikuwa ni Sh 521,709,523.65.

Anaeleza, hadi kufikia septemba 30, 2022 matumizi ya timu ni jumla ya Sh 493,431,406.25 na kusalia na Sh 28,278,117.38 kwenye akaunti ya timu.

Habari Zifananazo

Back to top button