Mageuzi kulibeba Soko la Kariakoo

SOKO la Kariakoo si tu eneo la kijiografia; ni injini ya kiuchumi na nguzo muhimu ya shughuli za kibiashara nchini Tanzania.

Likiwa na historia ndefu iliyobadilika kutoka kambi ya kijeshi hadi kuwa kitovu kikuu cha biashara, Kariakoo
inawakilisha uwekezaji wa kimkakati wa serikali katika miundombinu ya kibiashara.

Ukarabati na ujenzi mpya wa soko hilo ambao umekamilika unaashiria mustakabali wa biashara yenye ufanisi, uwazi na tija muhimu kwa ukuaji wa uchumi wa taifa anasema Meneja Mkuu wa soko hilo, Ashraph Abdulkarim.

Kariakoo ni hadithi ndefu ya kuanzia ukoloni. Jina Kariakoo lina mizizi yake katika matamshi ya wenyeji wa Dar es Salaam walioshindwa kulitamka vizuri jina la kambi ya kijeshi ya Wajerumani, ‘Carrier Corps’, iliyojengwa mwaka 1914.

Eneo hilo, lililokuwa ghala la silaha, lilibadilishwa matumizi na Waingereza mwaka 1919 na kuwa soko dogo la mazao ya chakula. Tangu hapo, Kariakoo lilijijengea umaarufu kama eneo muhimu la kibiashara, likihudumia mahitaji ya wakazi wengi wa Dar es Salaam.

Historia ya soko hilo inasema kuwa mwaka 1970, kutokana na ongezeko la mahitaji ya soko la kisasa, serikali iliamua kulijenga upya. Mradi huo ulikamilika Novemba 1975 na kuzinduliwa rasmi na Rais wa Awamu ya Kwanza wa Tanzania, Mwalimu Julius Kambarage Nyerere, Desemba 8, 1975.

Kuanzishwa kwa Shirika la Masoko ya Kariakoo mwaka 1974 kupitia Sheria ya Bunge Na 36 kulilenga kusimamia na kuendesha soko hilo, huku marekebisho ya sheria yakifanywa miaka ya 1985 na 2002 yakibainisha umiliki na mamlaka yake.

Abdulkarim anasema Kariakoo ni kitovu cha biashara ya jumla nchini na Bidhaa nyingi zinazoingia nchini huishia hapo kabla ya kusambazwa kwenda mikoa mingine na nchi jirani. “Hii inalifanya kuwa kiungo muhimu katika mnyororo wa ugavi likipunguza gharama za usambazaji na kuhakikisha upatikanaji wa bidhaa kwa wananchi wengi. Ufanisi wake unaathiri moja kwa moja bei za bidhaa sokoni,” anasema Abdulkarim.

Kutokana na historia na kwa mujibu wa Ofisa habari wa shirika hilo, Revocatus Kassimba, Kariakoo ya sasa inakwenda ikinyumbulika kulingana na mahitaji ya watu katika muda husika. Umuhimu wa kiuchumi Soko la Kariakoo si tu sehemu ya ununuzi na uuzaji wa bidhaa, bali ni mhimili mkuu wa shughuli za kiuchumi unaochangia kiasi kikubwa katika pato la taifa na ustawi wa jamii.

Zaidi ya hayo, soko hilo limeelezwa kuwa chanzo kikubwa cha ajira kwa maelfu ya Watanzania. Kuanzia wafanyabiashara wadogo na wakubwa, vibarua wa kubeba mizigo, madereva, watoa huduma za kifedha na usalama. Kariakoo hutoa fursa za kujipatia kipato.

Kukamilika kwa ukarabati na ujenzi wa soko jipya kunatarajiwa kuongeza zaidi ya ajira 4,000, jambo litakalochangia kupunguza tatizo la ukosefu wa ajira na kuongeza nguvu kazi yenye kipato. Sambamba na hilo, kupitia kodi za vizimba, ada za leseni za biashara na tozo mbalimbali, Soko la Kariakoo huchangia ongezeko la mapato ya serikali za mitaa na serikali kuu.

Mapato haya ni muhimu kwa ajili ya kufadhili miradi ya maendeleo ya umma kama vile ujenzi wa barabara, shule na hospitali. Ufanisi wa soko unahakikisha kuongezeka kwa msingi wa kodi na hivyo kuimarisha uwezo wa kifedha wa serikali.

Kukiwa na taarifa kwamba shirika lipo katika hatua za mwisho za maandalizi ya kuwarejesha wafanyabiashara katika Soko Kuu la Kariakoo baada ya kukamilika kwa mradi mkubwa wa ujenzi na ukarabati wa soko hilo ulioanza mwaka 2022, mradi ambao umegharimu Sh bilioni 28.03 likiwa na nafasi za biashara 1,907.

Tangu kukamilika kwa uhakiki wa wafanyabiashara waliokuwepo awali katika soko hilo, shirika linaendele kuwapanga wafanyabiashara 1,520 pamoja na wale waliopata maeneo ya biashara kupitia mnada katika mfumo wa Tausi kujiweka sawa ili kuendelea kuvutia zaidi wafanyabiashara kutoka nchi jirani za Afrika Mashariki na Kati.

Katika masuala ya maandalizi, Kassimba anasema menejimenti inafanya juhudi kubwa katika kuihakikisha kila kitu kiko sawa tayari kwa ufunguzi wa soko hilo.

Mmoja wa wafanyabiashara wa soko hilo, Sirio John anasema kuwa kwa sasa wakulima na wazalishaji wa bidhaa za chakula kutoka mikoa mbalimbali wana uhakika wa soko, jambo linalochochea uzalishaji wa mazao ya kilimo na viwanda vidogo nchini.

Kufuatia janga la moto la Julai 10, 2021, Serikali ya Awamu ya Sita, chini ya uongozi wa Rais Samia Suluhu Hassan ilitoa Sh Bilioni 28.03 kukarabati na kujenga upya Soko la Kariakoo. Uwekezaji huo si tu wa miundombinu, bali pia katika mifumo itakayohakikisha biashara inarejea kwa uhuru, uwazi na nidhamu ya hali ya juu.

Aidha, kukamilika kwa mradi wa ujenzi na ukarabati kumeleta soko lenye miundombinu bora, salama na inayokidhi mahitaji ya wafanyabiashara wa kisasa kwani usanifu wake umezingatia aina tofauti za biashara, kuhakikisha kila mfanyabiashara anapata nafasi inayomfaa na hivyo kuongeza ufanisi wa shughuli za kibiashara.

Pia, mkakati wa Shirika la Masoko ya Kariakoo kuingia katika mfumo wa kielektroniki wa Tausi (Tanzania Automated Unified System for Integrated Management) utaondoa malalamiko kwani unakuwa msingi wa kuimarisha utawala bora na nidhamu ya biashara.

Kupitia mfumo huu, wafanyabiashara wana jisajili na kupangiwa maeneo kwa uwazi, wakiona maeneo yao ya biashara na kupata hati za malipo kwa urahisi. Kasimba anasema hadi Mei 16, 2025, asilimia 76 ya wafanyabiashara (1,159 kati ya 1,520) wamepangiwa maeneo.

Anasema nafasi mpya za biashara zinatangazwa na kutolewa kwa njia ya mnada wa kidijiti, jambo linaloondoa upendeleo na kukuza ushindani wa haki na kuongeza kuwa hali hiyo inahakikisha kuwa maeneo yanapangishwa kwa wale wenye uwezo na utayari wa kufanya biashara, na hivyo kuongeza tija ya jumla ya soko hilo.

Pia, anasema ili kuhakikisha matumizi bora ya maeneo ya biashara, Shirika limeweka sera inayohitaji wafanyabiashara kulipa kodi na kufanya biashara aliyopangiwa. “Mtu yeyote atakayelipia eneo na kuliacha wazi bila kufanya biashara ndani ya miezi mitatu, atanyang’anywa eneo hilo.

Sera hii inalenga kuongeza tija ya matumizi ya nafasi na kuzuia ukodishaji holela, na hivyo kuongeza mzunguko wa biashara sokoni,” anasema Meneja Mkuu wa soko hilo.

Meneja Mipango na Biashara wa Shirika la Masoko ya Kariakoo, Mwinga Luhoyo anasema wanategemea ufanisi katika biashara sokoni hapo hasa kutokana na ushirikishwaji wa wadau na wafanyabiasahara katika kuhakikisha huduma bora.

“Shirika la Masoko ya Kariakoo liliratibu semina ya utoaji elimu kwa wafanyabiashara kwa kushirikiana na wadau na taasisi mbalimbali ikiwemo Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU), Shirika la Bima la Taifa (NIC), Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA), Benki ya Biashara (TCB), Jeshi la Zimamoto na Uokoaji na
Benki ya Taifa ya Biashara (NBC),” anasema Luhoyo.

Habari Zifananazo

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Back to top button