MAHAKAMA ya Hakimu Mkazi Kisutu imesema haiwezi kubadilisha mashariti ya dhamana katika kesi inayomkabili Mkurugenzi wa Kampuni ya Jatu, Peter Gasaya kwa kuwa mahakama hiyo imefungwa mikono na sheria na kama wana hoja kuhusu uamuzi huo waende Mahakama kuu.
Uamuzi huo umetolewa leo na Hakimu Mkazi Mkuu, Mary Mrio wakati kesi hiyo ilipoitwa kwa ajili ya kutolewa uamuzi wa maombi yaliyowasilishwa na upande wa utetezi ya kuomba kubadilishiwa masharti ya dhamana.
Mrio alisema mahakama hiyo imefungwa mikono kubadilisha masharti ya dhamana na kama watakuwa na hoja kuhusu uamuzi huo waende mahakama Kuu.
Baada ya kusema hayo Hakimu Mrio aliahirisha kesi hiyo hadi Machi 13, mwaka huu kwa ajili ya kutajwa.
Februari 16 mwaka huu kesi hiyo ilipoitwa kwa ajili ya upande wa mashtaka kujibu hoja za utetezi kutaka masharti ya dhamana yafanyiwe marekebisho, upande wa mashitaka ukiongozwa na wakili wa serikali, Caroline Matemu uliiomba mahakama hiyo kutupilia mbali ombi hilo kwa sababu mahakama haiwezi kutengua amri iliyojiwekea yenyewe.
Upande wa utetezi unaoongozwa na wakili Kung’he Wabeya waliwasilisha maombi kuitaka mahakama hiyo kulegeza masharti ya dhamana kwa kuwa masharti ya sasa ni magumu.
Katika kesi hiyo inadaiwa kuwa terehe isiyofahamika kati ya Januari mosi na Desemba 31, mwaka 2021 ndani ya mkoa wa Dar es Salaam, mshitakiwa akiwa Mkurugenzi Mtendaji wa Kampuni ya Jatu Public Limited, alijipatia Sh 5,139,865,733.00 kutoka Saccos ya Jatu, akijinasibu kukizalisha kiasi hicho cha fedha kwa kuwekeza fedha katika kilimo cha faida wakati akijua si kweli.