Majaji, mahakimu kupigwa msasa uhalifu mitandaoni
MAJAJI wa Mahakama Kuu Tanzania na Zanzibar, manaibu wasajili, mahakimu, waendesha mashtaka na wapelelezi watanufaika na ujuzi wa kukuza taaluma zako kupitia Kongamano la Kujadili Makosa ya Uhalifu Mtandaoni na Ushahidi wa Kielektroniki lililofunguliwa na Jaji wa Mahakama ya Rufani, Augustine Mwarija Dar es Salaam leo.
Mafunzo hayo yaliyoandaliwa na Chuo cha Uongozi wa Mahakama Lushoto (IJA) kwa kushirikiana na Sekretarieti ya Jumuiya ya Madola, yatafanyikwa kwa siku tatu kuanzia leo yakishirikisha majaji wa Mahakama Kuu 15, kutoka Bara na Visiwani, manaibu wasajili wanne, mahakimu 12, waendesha mashtaka wanane na wapelelezi saba.
SOMA: TCRA kudili na matapeli mitandaoni
Akizungumza katika ufunguzi wa mafunzo hayo kwa niaba ya Jaji Mkuu wa Tanzania, Profesa Ibrahimu Juma, Jaji Augustine Mwarija amesema mafunzo hayo yanaelenga kuimarisha ujuzi katika sheria ya uhalifu wa mtandaoni na kushughulikia ushahidi wa kielektroniki.
Amesema hatua hiyo ni mpango wa uhalifu wa Mtandao wa Sekretarieti ya Jumuiya ya Madola kuunga mkono utekelezaji wa Azimio la Mtandao la Jumuiya ya Madola (CCD) la 2018 linaonesha juhudi za Sekretarieti ya Jumuiya ya Madola kupunguza kiwango na athari za uhalifu wa mtandaoni nchini.
Amesema wajumbe watachunguza mienendo ya kimataifa, kikanda, na ya ndani katika uhalifu wa mtandaoni, kuongeza uelewa wao wa sheria zinazosimamia makosa ya mtandaoni, na kujadili changamoto za kiutendaji zinazokabili katika kuchunguza, kuendesha mashtaka na kutolea uamuzi kesi.
SOMA: 94 wakamatwa Tanga makosa ya uhalifu
Jaji Mwarija amesema Tanzania hakuna namba kubwa ya makosa ya kimtandao, lakini kadri teknolojia inavyokuwa, uhalifu pia unaongezeka hivyo ni muhimu kuchukua hatua za mapema kukabiliana na changamoto hiyo.
“Kwa bahati nzuri hatuna kesi nyingi kwa sasa, lakini kadri teknolojia inavyozidi kukuwa na uhalifu unaongezeka, lakini pia kutakuwa na mada mbalimbali,” amesema Mwarija.
Mkuu wa Chuo cha Uongozi wa Mahakama Lushoto (IJA) ambaye ni Jaji wa Mahakama ya Rufani, Dk Faustine Kihwelo amesema mafunzo hayo yatawajengea uwezo wahusika namna ya kukabiliana na uhalifu wa mitandao na ushahidi wa kielektroniki.
“Ndio maana tumewaleta wapelelezi, kwa sababu makosa yakitokea anayeanza kufanya kazi ni mpelelezi, lakini akimaliza jarada linaenda kwa muendesha mashtaka, na mwisho wa siku yanaletwa mahakamani, hivyo tunawaleta hawa watatu ili wawe na uelewa wa pamoja,” amesema Dk Kihwelo.
Amesema wahalifu wengi wanatumia njia ya mitandao tofauti na njia zingine, hivyo kongamano hilo litatoa ujuzi kwa wahusika namna ya kukabiliana na changamoto hiyo.