Majaji washauriwa kutafuta suluhu ya wakimbizi Afrika

RAIS wa Mahakama ya Afrika ya Haki za Binadamu na Watu, Jaji Imani Aboud amesema ipo haja ya Chama cha Majaji wanaoshughulikia masuala ya wakimbizi na wahamiaji Afrika kutafuta suluhu ya migogoro inayochangia uwepo wa wahamiaji katika nchi za Afrika na kuweza kuja na suluhisho lake.

Jaji Imani alisema hayo jijini Arusha jana wakati akizungumza kwenye Mkutano wa Chama cha Majaji wanaoshughulikia Masuala ya Wakimbizi na Wahamiaji Afrika (IARMJ).

Alisema kuwepo kwa wahamiaji katika nchi za Afrika kumekuwa kukichangiwa na uwepo wa migogoro ya kisiasa pamoja na mabadiliko ya tabianchi, ambayo husababisha wananchi wengi kukimbia nchi zao kwenda nchi zingine kutafuta amani.

Alisema kutokana na changamoto hizo ni lazima nchi za Afrika zijitafakari na kutafuta suluhu ya changamoto hizo ambazo zinachangia wahamiaji hao kutoka nchi moja kwenda nchi nyingine.

“Lazima tuangalie vyanzo vinavyosababisha kuwepo kwa wakimbizi na wahamiaji hao na tuweke mikakati ni namna gani ya kuondokana na changamoto hizo na tuwaangalie ndugu zetu hawa kwa jicho la huruma na haki za watu kwani wanavyofanya hivyo haifanyi makusudi bali ni mazingira ndio yanachangia wao kufanya hivyo,” alisema.

Pia alifafanua kuwa ni vizuri wakajadili kwa pamoja kuangalia migogoro ya kisiasa inaathiri vipi nchi za Afrika na kuja na mikakati ya kukabiliana na migogoro hiyo, huku kwa upande wa mabadiliko ya tabianchi waangalie namna ya kujipanga mapema katika kukabiliana na mabadiliko hayo.

Naye Rais wa IARMJ, Jaji Isaac Lenaola alisema lengo la mkutano huo ni kupanua uelewa wa masuala ya wakimbizi kwa maofisa wa serikali, majaji, mahakimu na watoa maamuzi wengine Afrika.

Jaji Lenaola alisema kupitia mkutano hao majaji hao watazungumzia kuhusiana na haki za wahamiaji na kuangalia namna ya kukabiliana na changamoto zinazowakabili na kuwafanya kukimbia nchi zao ikiwemo mabadiliko ya tabia ya nchi.

Habari Zifananazo

Back to top button