Majaliwa ahadharisha matumizi akili mnemba sekta ya afya

WAZIRI Mkuu, Kassim Majaliwa amewataka wataalamu wa afya nchini kuhakikisha matumizi ya teknolojia katika sekta ya afya ikiwemo akili mnemba hayaathiri usalama, huduma na ulinzi wa taarifa.
Alisema matumizi ya kidijiti yanapaswa kuwasaidia wataalamu wa afya kubaini na kutambua aina mbalimbali za magonjwa mapema, kutibu na kufuatilia maendeleo ya mgonjwa.
Aliyasema hayo jana kwenye kongamano la 13 la kisayansi lililofanyika katika Kituo cha Umahiri wa Magonjwa ya Moyo Afrika Mashariki, Mloganzila Dar es Salaam.
Kongamano hilo la siku mbili limeandaliwa na Chuo Kikuu cha Afya na Sayansi Shirikishi Muhimbili (MUHAS) lenye kaulimbiu, “Kubadili Mifumo ya Afya Afrika: Kuweka kipaumbele katika bunifu na tafiti katika kukabiliana na changamoto nyumbufu za afya duniani’’.
Majaliwa alisema serikali itaendelea kuwekeza katika vifaatiba, teknolojia, miundombinu na rasilimaliwatu kukabiliana na magonjwa ya mlipuko na kuboresha sekta ya afya.
Alielekeza wataalamu kuendelea kuwekeza katika tafiti zenye tija kwa wananchi na matokeo yake yaonekane katika mabadiliko ya sera na mipango.
Aliongeza: “Vyuo vikuu na taasisi ni lazima mzalishe wataalamu wabobezi sambamba na kuwekeza katika tafiti zenye tija kwa wananchi, waone matokeo katika utoaji wa huduma za afya zinazoendana na kasi ya mabadiliko ya teknolojia’’.
Kwa upande wake, Naibu Katibu Mkuu, Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia, Profesa Daniel Mushi alisema uwekezaji unaoendelea kufanywa na serikali katika chuo hicho unachochewa na matokeo chanya yanayooneshwa.
“Chuo hiki kimefanikiwa kuingia miongoni mwa vyuo vitano bora katika Ukanda wa Kusini mwa Jangwa la Sahara, ushahidi wa ubora wa mafunzo, tafiti zenye tija, na weledi wa hali ya juu wa wakufunzi wake,’’ alisisitiza.
Kwa upande wake, Makamu Mkuu wa chuo cha Muhas, Profesa Appolinary Kamuhabwa alisema katika kongamano hilo, mawasilisho 200 ya tafiti yatafanywa kwa njia ya maongezi na kwa njia ya mabango.
Pia, mawasilisho hayo yatafanywa na washiriki kutoka ndani na nje ya nchi takribani 218 kutoka mataifa mbalimbali yakiwemo Tanzania, Kenya, Marekani, Norway na Zambia.
“Mawasilisho ya tafiti hayo ni katika magonjwa yasiyo ya kuambukiza, magonjwa ya kuambukiza na usugu wa vimelea vya magonjwa, afya ya mama, mtoto na kijana, tiba mbadala na tafiti za chanjo,’’ alisema Profesa Kamuhabwa.
Pia, alieleza tafiti nyingine ni katika afya ya kinywa, macho, masikio, pua na koo, akili mnemba, teknolojia na usalama na afya kazini pamoja na utafiti wa mifumo ya afya na afya jumuishi.