Majaliwa ateta na Waziri Mkuu wa Côte d’Ivoire

WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa amekutana na Waziri Mkuu wa Côte d’Ivoire, Robert Beugre Mambe na kujadiliana naye masuala ya kidiplomasia, kiuchumi, teknolojia, kilimo na michezo kwenye kikao kilichofanyika ofisini kwa mwenyeji wake, Boulevard Angoulvant Plateau, jijini Abidjan.
Akitoa ufafanuzi mara baada ya kikao hicho Waziri Mkuu Majaliwa amesema lengo la kikao chao lilikuwa kuimarisha mahusiano ya kidiplomasia lakini pia kuhimiza haja ya nchi hiyo kushirikiana na Tanzania kwenye masuala mbalimbali ikiwemo utafiti na teknolojia za kisasa kwenye kilimo.
“Côte d’Ivoire ina wakazi zaidi ya milioni 81 na inaongoza kwa kilimo cha kakao, korosho na michikichi. Hawa wanalima korosho zaidi kuliko Tanzania, na sisi tunalima korosho kwenye mikoa ya Pwani na kakao kule Mbeya na maeneo mengine,” amesema.
“Kakao ni zao kuu la biashara na linawaingiza fedha nyingi za kigeni. Tumekubaliana kuwa mawaziri wetu wa kilimo wakutane na waangalie ni maeneo gani ya kuweka mikataba ikiwemo utafutaji wa masoko na masuala ya utafiti,” amesema Waziri Mkuu Majaliwa ambaye alikuwa Abidjan kumwakilisha Rais Samia Suluhu Hassan katika jukwaa la siku mbili la Maafisa Watendaji Wakuu barani Afrika.
Majliwa amesema wamekubaliana kuwa jukwaa hilo lifanyike mapema ili wafanyabiashara wa pande hizo mbili wakutane na kubadilishana mbinu na kwamba sekta binafsi ilisimamie eneo hilo.
Mapema, Waziri Mkuu wa Côte d’Ivoire, Robert Beugre Mambe ambaye pia ni Waziri wa Michezo na Ustawi wa Jamii, alimpongeza Rais Samia kwa hatua kubwa aliyofikia katika kuiongoza Tanzania huku akiipongeza Tanzania kwa kuandaa mkutano mkubwa wa nishati Afrika uliofanyika Januari 27 hadi 28.
“Tunatarajia kushirikiana nanyi kwenye masuala ya zana za kisasa za kilimo. Teknolojia ya kilimo huku kwetu iko juu sana na tunasubiri kuanza kwa jukwaa la wafanyabiashara ili watu wetu waweze kubadilishana uzoefu,” asema Mambe.

Habari Zifananazo

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Back to top button