Majaliwa aweka jiwe la msingi Shule ya Sekondari Dk Samia

WAZIRI Mkuu Kassim Majaliwa leo Januari 6, 2023 ameweka jiwe la msingi la ujenzi wa shule ya sekondari ya wasichana ya Dk Samia Suluhu Hassan iliyopo wilaya ya Namtumbo mkoani Ruvuma.

Mradi huo unatekelezwa kwa awamu mbili kwa gharama ya shilingi bilioni 4 kupitia Mradi wa Kuboresha Elimu ya Sekondari (SEQUIP),  ambapo Awamu ya Kwanza ya mradi huu ilianza tarehe April 6, 2022 na inatarajiwa kukamilika Januari 30, 2023 utatumia shilingi bilioni 3 na jumla ya majengo 22 yanajengwa.

Majaliwa amesema shule hiyo itakapokamilika itapokea wanafunzi 1080, ambapo awamu ya kwanza itapokea wanafunzi 600.

Awamu ya pili ambayo ujenzi wake unatarajiwa kuanza ndani ya mwaka huu kwa gharama ya shilingi bilioni 1 inatarajiwa kupokea wanafunzi 480 pale itakapokamilika

Awamu ya pili itahusisha ujenzi wa madarasa 10 yenye ofisi za walimu 3, chumba cha ICT, maktaba, nyumba 4 za walimu na mabweni 4.

Waziri Mkuu Majaliwa amesema kuwa Dk Samia ameamua kuwekeza kwenye elimu ya mtoto wa kike, ili kumpunguzia changamoto zinazowakabili na ndio maana ameamua kujenga shule za wasichana nchi nzima.

“Si kwamba amemtenga mtoto wa kiume hapana, ameamua kwenda nao wote,” amesema.

Pia Waziri Mkuu amewataka wakandarasi wanaojenga shule hiyo kuhakikisha wanakamilisha ujenzi wa shule hiyo katika muda uliopangwa, ili waanze kupokea wanafunzi.

Shule ya Sekondari  Dk Samia Suluhu Hassan inatarajia kuanza kupokea wanafunzi wa kidato cha tano Julai, 2023.

Naye Naibu Waziri Ofisi ya Rais (TAMISEMI) Dk Festo Dugange amesema watahakikisha wanasimamia ujenzi wa miundombinu iliyobaki katika shule hiyo, ili ikamilike na ianze kudahili wanafunzi

 

Habari Zifananazo

Back to top button