Majaliwa: Tutaendelea kuboresha uwekezaji

SERIKALI imesema itaendelea kuweka mazingira mazuri kwa wawekezaji kutekeleza ahadi katika ilani ya uchaguzi ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) ya kuendelea kutoa fursa za ajira kwa wananchi kupitia sekta ya viwanda.

Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa amesema hayo alipotembelea kiwanda cha kuzalisha saruji cha Maweni Limestone mkoani Tanga. Majaliwa alisema nia ya Rais Samia Suluhu Hassan ni kuendelea kutengeneza fursa za uwekezaji kupitia maeneo mbalimbali vikiwemo viwanda ikiwa ni maelekezo yaliyopo kwenye ilani ya uchaguzi ya CCM.

“Tunataka mwakani tunapokwenda kuomba ridhaa kwa viongozi wa vijiji basi Chama Cha Mapinduzi kitembee kifua mbele kutokana na namna ambavyo serikali ya awamu ya sita ilivyoweza kutekeleza ilani hiyo kwa vitendo,” alisema.

Advertisement

Mkuu wa Mkoa wa Tanga, Waziri Kindamba alisema mazingira mazuri ya uwekezaji yaliyowekwa na serikali katika mkoa huo yamesaidia kuongeza idadi ya viwanda vikubwa kutoka 16 mwaka 2015 hadi kufikia 25 mwaka huu.

“Viwanda vya kati vimeweza kuongezeka kutoka viwanda 23 mwaka 2015 hadi kufikia viwanda 76 mwaka huu huku viwanda vidogo vidogo navyo vikikuwa kwa kasi kutoka viwanda 440 hadi kufikia 1414,” alisema Kindamba.

Aidha aliwataka wawekezaji wengine waone umuhimu wa kuwekeza katika mkoa huo kwa kuwa ni salama kwa ajili ya mitaji yao. Mbunge wa jimbo la Tanga Mjini, Ummy Mwalimu aliiomba serikali iangalie uwezekano wa kumaliza mgogoro wa ardhi katika eneo hilo la kiwanda cha Maweni na wananchi ambao wamevamia eneo la mwekezaji.

“Mgogoro wa ardhi uliopo unasababisha mwekezaji kushindwa kuendelea na uwekezaji katika eneo hilo jambo ambalo halileti sifa nzuri “alisema Ummy.

Meneja wa kiwanda hicho, James Gin alisema mahitaji wa saruji ni makubwa nchini hivyo uwekezaji wao utaongeza chachu ya uzalishaji wa saruji bora.

“Uwezo wa kiwanda chetu ni kuzalisha zaidi ya tani milioni mbili kwa mwaka lakini iwapo changamoto ya makaa ya mawe itaweza kutafutiwa ufumbuzi tunaweza kuongeza uwezo wa uzalishaji wa saruji katika kiwanda chetu,” alisema Gin.

/* */