Majaliwa: Tutaendelea kuwalinda, kuwapatia fursa stahiki watu wenye ulemavu

WAZIRI Mkuu, Kassim Majaliwa amesema kuwa Serikali ya awamu ya sita inayoongozwa na Rais Samia Suluhu Hassan inawathamini watu wenye ulemavu wakiwemo wenye ualbino na wakati wote itahakikisha inawalinda na kuwapatia fursa stahiki katika ujenzi wa Taifa.
Amesema katika kuendelea kutekeleza mpango wa uwezeshaji wananchi kiuchumi kwa kutumia mikopo inayotokana na mapato ya ndani ya Halmashauri, hadi kufikia Machi, 2025 tayari shs bilioni 5.48 zimetolewa kwa vikundi 891 vya Watu Wenye Ulemavu nchini.
Amesema kuwa Serikali itaendelea kuchukua hatua mahsusi za kuimarisha ustawi na utoaji huduma kwa watu wenye ualbino ikiwemo kuwatambua, kuimarisha mifumo ya kisera na kuwezesha upatikanaji wa huduma muhimu hapa nchini.
Ametoa kauli hiyo leo Juni 13, 2025 wakati alipomuwakilisha Rais Samia kwenye kilele cha Maadhimisho ya Siku ya Kimataifa ya Uelewa kuhusu Ualbino yaliyofanyika katika uwanja wa Mwanga Centre, mkoani Kigoma.
Ameongeza kuwa katika mwaka 2024/2025 kiasi cha ruzuku inayotolewa kwa Vyama vya Watu wenye Ulemavu kimeongezeka hadi kufikia shs milioni 230 ikilinganishwa na shs milioni 200 zilizotolewa kwa mwaka 2023/2024.
Akizungumza kuhusu kuimarika kwa utoaji wa huduma za afya kwa watu wenye Ualbino, Majaliwa amesema kuwa kwa kipindi cha kuanzia Julai 2021 hadi Juni 2024 Serikali kupitia Bohari Kuu ya Dawa (MSD) ilitumia zaidi ya shs milioni 500 kusambaza katika mikoa yote 26 ya Tanzania mafuta kinga ya saratani ya ngozi kwa Watu wenye Ualbino.
“Kwa mwaka wa fedha 2024/2025, Serikali ilitenga shilingi bilioni 8.743 kwa ajili ya huduma za ustawi wa Jamii na shilingi 182. 8 kwa ajili ya ununuzi wa mafuta kinga ya saratani ya ngozi kwa watu wenye Ualbino,” amesema Majaliwa.

Habari Zifananazo

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Back to top button