Majaliwa: Viongozi wa dini kemeeni uvunjifu wa maadili, amani

WAZIRI Mkuu, Kassim Majaliwa amewaomba viongozi wa dini kuendelea kukemea uvunjifu wa maadili sambamba na kuliombea amani taifa hasa katika kipindi hiki cha kuelekea Uchaguzi Mkuu 2025.

Rai hiyo ameitoa wakati wa Baraza la Maulid ya kumbukumbu ya kuzaliwa Mtume Muhammed (S.A.W) yaliyofanyika kitaifa wilaya ya Korogwe mkoani Tanga, ambapo amesema viongozi hao kauli zao zina nguvu kubwa katika jamii.

Amewataka kuendelea kukemea na kutofumbia macho vitendo vya uvunjifu wa maadili ambavyo vinaendelea katika jamii hasa katika kipindi hiki cha kuelekea katika uchaguzi.

“Serikali tutaendelea kuunga mkono taasisi za dini ikiwemo viongozi hao kuanzia ngazi za msingi hadi taifa kwani kwa kufanya hivyo tunakwenda kujenga msingi wa kujadili jambo kwa pamoja na kulipatia ufumbuzi wa pamoja,” amesema.

SOMA: Watanzania wahamasishwa kutunza amani

Kwa upande wake, Mufti wa Tanzania, Shehe Dk Abubakar Zuberi amewataka viongozi wa dini kwenye maeneo yao kuhakikisha wanasimamia amani hasa katika kipindi cha kuelekea kwenye uchaguzi mkuu.

Amewataka kutofumbia macho vitendo vyote ambavyo vinaashiria hali ya uvunjifu wa amani kwenye maeneo yao.

Amesema kwa kufanya hivyo watakuwa wametimiza lengo la dini na mafundisho ya Mtume Muhammed (S.A.W).

Amewataka waumini wa dini ya Kiislamu kujitokeza kusikiliza sera za wagombea wa vyama na kushiriki katika kupiga kura wakati wa uchaguzi ili kupata viongozi ambao wataweza kuleta maendeleo.

“Asibakie mtu hata mmoja nyumbani na tuiombee sana dua nchi yetu hasa katika kipindi hiki cha uchaguzi kwani amani ndiyo msingi wa maendeleo, hivyo ni muhimu tunu hii tukaienzi na kuilinda,” amesema.

Katibu Mkuu wa Bakwata, Nuhu Mruma ameonya watu wenye tabia ya kuwatukana na kuwakashifu viongozi na walio na joto la jazba la kisiasa akiwataka kuacha tabia hizo.

Amesema kupitia mitandao ya kijamii, mmomonyoko wa maadili unaendelea kushuhudiwa ambapo baadhi ya watu huwatukana na kuwakashifu viongozi mbalimbali kinyume na ustaarabu wa kawaida na utu.

“Tunawaasa ndugu zetu wanaofanya mambo hayo waache matusi kwani wajue kuwa wanapata dhambi kubwa na hakuna faida yoyote wanayoipata zaidi ya hasara ya dhambi. Wajibu wetu kama raia ni utiifu kwa viongozi na kushauri pale ambapo unaona panahitaji kufanya hivyo,” ameshauri.

Wakati nchi ikiendelea na michakato mbalimbali ya uchaguzi zikiwemo kampeni, alisema baraza hilo linahamasisha waumini wao na wananchi kwa ujumla kushiriki kikamilifu na kuhudhuria mikutano ya kampeni kwa vyama vyote vilivyoruhusiwa na Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi (INEC) kushiriki uchaguzi huo.

“Tupunguze joto la jazba za kisiasa na tujilazimishe kufuata taratibu sahihi zilizowekwa na tume ya uchaguzi (Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi – INEC) katika utatuzi wa changamoto zozote za uchaguzi zitakajitokeza katika kipindi hiki cha mpito. Tunawaomba waende kuwasikiliza wagombea na sera zao na kuuliza maswali endapo sheria za uchaguzi zinaruhusu kufanya hivyo,” ameeleza.

Pia baraza hilo limewasihi Waislamu na wananchi kwa ujumla kuzingatia misingi ya amani na utulivu katika mchakato mzima wa uchaguzi huo na kufuata maelekezo ya taratibu na sheria yanayotolewa na wasimamizi na maofisa wa INEC siku ya kupiga kura itakapowadia.

“Tunawaomba wasimamizi na waratibu wa uchaguzi mkuu watekeleze majukumu yao kwa weledi na kufuata sheria zinazoongoza mchakato mzima wa uchaguzi huo. Kufanya hivyo kutapunguza malalamiko, hivyo kuufanya uchaguzi kufikia lengo la kuwa uchaguzi huo ni wa huru na haki,” ameongeza.

Imeandikwa na Amina Omary, Korogwe na Lydia Inda, Dar.

Habari Zifananazo

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Back to top button