Kaya 413 zazingirwa maji Ziwa Victoria

SIMIYU: Kaya 413 katika Kijiji cha Lamadi Wilaya ya Busega mkoani Simiyu zimekosa makazi baada ya nyumba zao kuzingirwa na maji yalitokana na kujaa kwa Ziwa Victoria athari za mvua zinazoendelea kunyesha nchini.

Mkuu wa Wilaya hiyo, Faiza Salim amethibitisha kuwepo wa athari hizo, ambapo ameeleza hatua ambazo wamechukua ili kunusuru maisha ya wananchi wa kijiji hicho ni kutenga maeneo ya shule kwa ajili ya wananchi hao kwenda kujihifadhi.

” Tumetenga maeneo ya Shule ya Sekondari Anthony Mtaka, Shule ya Msingi Lamadi, Shule ya Msingi Lukungu kwa ajili ya wananchi hao kwenda kujihifadhi huku tukisubiria maji yarudi ziwani, lakini pia tumeomba msaada wa chakula kutoka serikali kuu na mahitaji mengine kwa ajili ya afya za wananchi,” amesema Faiza.

Mwenyekiti wa kijiji hicho, Elias Sangoma na Diwani wa kata hiyo Bija Laurenti wamesema athari ambazo zimejitokeza ni nyumba kujaa maji, vyoo kujaa maji na kuhatarisha mlipuko wa kipindi pindu, pamoja na vyakula kuloana na wananchi kukosa chakula.

Ester Yohana mmoja wa wananchi walioathirika na maji hayo, amesema changamoto iliyopo ni wao kukosa huduma muhimu za chakula na afya huku uwepo wa baridi kali ukiwatesa watoto wao.

” Kwa sasa kinachotutesa zaidi ni baridi hasa nyakati za usiku kwa watoto wetu, tunahofia wanaweza kupata nimonia, lakini vyoo sasa hivi vyote vimejaa maji tunaweza kupata mlipuko wa magonjwa, tunaomba serikali itusaidie,” amesema Ester.

 

Habari Zifananazo

Back to top button