Makala: Mgao wa maji Dar, Pwani Bye bye

MKUU wa Mkoa wa Dar es Salaam Amos Makala ametangaza kusitishwa rasmi kwa mgao wa maji katika Mkoa wa Dar es Salaam na Pwani.

Pia amemtaka Mbunge wa kiteuliwa. Dkt  Bashiru Ali Kakurwa kuacha kiranga kama hawezi kumsemea mazuri Rais Samia Suluhu Hassan ni bora akakaa kimya.

Advertisement

Makala ameyasema hayo leo Novemba 25,2022 katika ziara ya kukagua hali ya maji katika vyanzo vya Ruvu chini.

“Kwa wiki mbili, tatu hali ya maji Mkoa wa Dar es Salaam na Pwani kulikua na uhaba kutokana na ukame, serikali imefanya jitihada kubwa kuondoa watu maeneo ya vyanzo kwenye milima ya Uluguru na Pwani, mvua zimeanza kuonyesha na sasa hali ya maji ni nzuri ” Amesema Makala na kuongeza

“Kwa sasa Mkoa wa Dar es Salaam na Pwani unapata maji ya kutosha na ya ziada, uzalishaji wa maji wa awali ni Lita milioni 520, na uzalishaji wa maji kwa sasa ni Lita milioni 590.”Amesema Makala

Uhitaji wa maji wa Dar es Salaam na Pwani ni Lita milioni 544

Makala amesema  pia kuna ongezeko la maji la Lita milioni 70 kutoka Kigamboni na kufufuliwa kwa visima 20 kumefanya kuwa na idadi ya visima 169  ambavyo vina zalisha maji Lita milioni 31.9.

“Tunamshukuru Rais Samia Suluhu kwa kutoa fedha shilingi bilioni 24 katika mradi wa maji wa Kigamboni, tulipita kwenye kipindi kigumu, Mheshimiwa Rais alikua bega kwa bega na sisi kuhakikisha tunatumia kila njia wananchi wapate maji.

” Yapo mambo mengi mazuri Rais anayafanya, kelele za Dk Bashiru ni kiranga chake tu, akate simu, sisi tupo ‘ site’ kama ana nyongo yake ya chuki ale ndimu na malimao, aache sisi tuendelee kutangaza mazuri ya serikali  chini ya Jemedari wetu Rais Samia Suluhu Hassan.” Amesema.

Dkt. Bashiru akizungumza na Wakulima hivi karibuni alitoa kauli zinazodaiwa kukosoa Serikali, jambo lililofanya akemewe vikali huku wengine wakimtaka ajiuzulu Ubunge.

Wakati huo huo, Makala ameielekeza Mamlaka ya Maji Safi na Usafi wa Mazingira (Dawasa), kumalizia miradi ya pembezoni ukiwemo wa Mshikamano ambao unapeleka maji kwenye maeneo ya Kata ya Mbezi, Kibamba, Msakuzi, Madale na Mpiji Magoe.

Pia mradi wa kusambaza maji wa Makongo hadi Bagamoyo unaonufaisha wakazi wa Mabwepande, Bunju, Mbweni, Wazo, Tegeta A, Goba na Makongo.

Kwa upande wa Afisa Mtendaji Mkuu wa Dawasa, Cyprian Luhemeja amesema kuna ongezeko la maji Lita milioni 46.

“Ruvu Juu inazalisha Lita za maji milioni 166, Ruvu chini Lita milioni 270 ukichanganya na visima tunakua na maji Lita milioni 590, mahitaji ya Dar es Salaam na Pwani ni Lita milioni 544, hivyo maji yapo ya kutosha na ziada.” Amesema

Aidha, Luhemeja amewashukuru viongozi wa dini na kudai kuwa kujaa kwa maji kwenye vyanzo hivyo ni miujiza.

“Tumepita kipindi kigumu, binafsi naona kilichofanyika ni miujiza, tunawashukuru viongozi wa dini hawakutuacha, tunawashukuru pia wakazi wa Jiji la Dar es Salaam na Pwani kwa uvumilivu katika kipindi chote cha mgao .”,Amesema