Makamu wa Rais Ashiriki Mkutano wa AU-EU Angola

MAKAMU wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dk Emmanuel Nchimbi, ameshiriki Mkutano wa 7 wa Viongozi wa Umoja wa Afrika na Umoja wa Ulaya (AU-EU Summit), uliofanyika Luanda, Angola, tarehe 25 Novemba 2025.
Mkutano huo wa siku mbili ulijikita katika kuunda mustakabali endelevu wa Afrika na Ulaya, kuimarisha amani, usalama na utawala, pamoja na kushughulikia migogoro na vita kote ulimwenguni. Vilevile, viongozi wamezungumzia ushirikiano katika uhamiaji, maendeleo ya kiuchumi, viwanda, masoko ya kikanda, na utekelezaji wa Eneo Huru la Biashara la Bara la Afrika (AfCFTA).

Mkutano huo umeweka mkazo katika kukuza maendeleo endelevu, ushirikiano wa kibiashara na kiufundi, na utunzaji wa rasilimali asilia kwa njia ya kijani, huku ukidhamiria kushughulikia changamoto za mabadiliko ya tabianchi. Pia, umeadhimisha miaka 25 ya ushirikiano kati ya Umoja wa Afrika na Umoja wa Ulaya.
Makamu wa Rais Dk Nchimbi ameambatana na Waziri wa Kazi na Uwekezaji Serikali ya Mapinduzi Zanzibar, Dk Sharif Sharif, Naibu Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Dk Ngwaru Maghembe, pamoja na mabalozi na wataalamu wa serikali. SOMA: ‘Urani ya Namtumbo, mwanga mpya Tanzania kuelekea uchumi wa kisasa’



