Malipo ya korosho yafanyike vyama vikuu vya ushirika

SERIKALI imeendelea kusisitiza kuwa malipo yote ya wakulima wa korosho yafanyike kupitia vyama vikuu vya ushirika katika msimu wa kilimo mwaka 2024/2025.

Akizungumza leo mkoani Mtwara, Mrajisi na Mtendaji Mkuu kutoka Tume ya Maendeleo ya Ushirika Tanzania (TCDC), Dk Benson Ndiege amesema maelekezo hayo yametolewa na Rais Samia Suluhu Hassan.

Advertisement

Rai hiyo imetolewa wakati wa kikao cha wadau mbalimbali wa korosho wakiwemo viongozi wa vyama vikuu vya ushirika kutoka mikoa minne inayozalisha korosho nchini ikiwemo Pwani Ruvuma, Lindi pamoja na Mtwara.

Kikao hicho kimefanyika katika Manispaa ya Mtwara Mikindani mkoani Mtwara kilichohusu tathimini juu ya mchakato mzima wa mauzo au minada ya korosho ghafi yanavyoendelea katika msimu huo.

Amesema katika mfumo huo ambao ni mpya mpaka sasa wamefanikiwa kwa zaidi ya asilimia 80 na lengo ni kufikia asilimia 100 ya mfumo huo.

“Kwanza nipongeze kwamba hamna chama chochote cha msingi ambacho mwaka huu kimejishughulisha na malipo, malipo yote yanafanyika katika ngazi ya ushirika na niwapongeze sana kwa kusimamia maelekezo haya,”amesema Benson

Mkurugenzi Mkuu wa Bodi ya Korosho Tanzania (CBT), Francis Alfred amesema mpaka sasa zaidi ya tani 200,000 za korosho ghafi zimeshauzwa katika msimu huo kupitia minada mbalimbali ya korosho iliyofanyika kwenye maeneo mbalimbali, zenye thamani ya zaidi ya Sh bilioni 900.

Aidha kati ya fedha hizo zaidi ya Sh bilioni 800 zimekwenda kwa wakulima wa zao hilo huku akiviomba vyama vikuu hivyo kuwa, waweke watu ambao watapiga simu kwenye chama cha msingi (Amcos) ili kuulizia kama wakulima wote wamepata malipo yao ili kuondokana na changomoto zisizokuwa za lazima zinazoweza kujitokeza juu ya malipo hayo.