WAZIRI Mkuu Kassim Majaliwa amesema kuwa mapambano dhidi ya rushwa si jukumu la Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa(TAKUKURU) pekee bali kila Mtanzania anapaswa kushiriki kikamilifu kusimamia maadili na kupinga vitendo vya rushwa.
Amesema kuwa rushwa inaweza kusababisha kutofikiwa kwa jukumu la Serikali la kuleta ustawi wa wananchi linalotamkwa katika Ibara ya 8(1)[b] ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
Majaliwa amesema hayo leo Oktoba 26 alipomwakilisha Rais Dk. Samia Suluhu Hassan katika hafla ya ufungaji wa mafunzo ya awali ya uchunguzi ya TAKUKURU, yaliyofanyika kwenye Shule ya Polisi Tanzania, Moshi mkoani Kilimanjaro.
SOMA: Takukuru yabaini kasoro miradi 171
“Hili ni jukumu la kila Mtanzania na wadau wote muhimu hapa nchini, rushwa ni adui wa haki na maendeleo katika jamii, Vitendo vya rushwa rushwa vinasababisha uchepushaji wa rasilimali kutoka kwenye matumizi sahihi na kuathiri haki za kiraia,” amesema.
Pia, Majaliwa ameagiza TAKUKURU iongeze kasi na mikakati ya kudhibiti rushwa hasa katika maeneo ya ukusanyaji mapato, manunuzi wa umma, michakato ya ajira katika utumishi wa umma, mifumo ya ugawaji wa ardhi, utoaji wa huduma za jamii.