Mapato SGR yafika bil 28/- miezi minne

DAR ES SALAAM; SHIRIKA la Reli Tanzania (TRC) limesema usafiri wa treni ni biashara kubwa, hivyo haliwezi kuruhusu kushindwa kuifanya.

Mkurugenzi Mkuu wa TRC, Masanja Kadogosa alisema hayo jana asubuhi alipozungumza katika kipindi cha Clouds 360 kilichorushwa na kituo cha televisheni ya Clouds cha Kampuni ya Clouds Media ya Dar es Salaam

“Kwa mara moja inaposimama treni ni watu karibia 5,000 wanasubiria sio wanaondoka kuendesha magari wanasubiri imekuwa ni treni ya wananchi, hii ndiyo kipimo kwamba kwenye hiki kitu hatuwezi kufeli kwa sababu kwamba hatuwezi kuendeleza,” alisema Kadogosa.

Advertisement

Alisema hadi mwishoni mwa Novemba, mwaka huu walikuwa wamesafirisha watu milioni 1.1 na zaidi na kuwa ndani ya muda wa miezi minne walikuwa wamekusanya zaidi ya Sh bilioni 28 kutokana na mapato ya treni za reli ya kisasa (SGR).

Kadogosa pia alisema wananchi wamekuwa na mwamko mkubwa na mara nyingi treni zinakuwa zinajaa wakati wa safari za kuanzia Ijumaa hadi Jumatatu na kuanzia Jumanne hadi Alhamisi wanaosafiri wanakuwa kati ya asilimia 50, 60 hadi 80.

“Kwa mfano wakati tuliopata matatizo ya kiufundi yaliyotokea tulikuwa na treni nne zipo njiani moja ilikuwa Soga nyingine Ngerengere nyingine ilikuwa Morogoro nyingine Dar es Salaam, hapo unazungumzia zaidi ya watu kama 4,000 wapo barabarani inamaanisha ni biashara kubwa sana watu wameacha magari yao ndege wamehamia kwenye treni,” alisema.

Kadogosa alisema inasikitisha kuna watu wanaofanya njama za kurudisha nyuma uwekezaji huo na kuwa waliwakamata baadhi ya watu waliohusika, wakiwemo watoto wengine wa miaka 12 wengine 16 na wengine waliohusika kukata nyaya wakiwa ni watu wazima.

“Kuna kesi inaendelea kuna waliokamatwa wakikata nyaya na kesi inaendelea na pia zingine tunaendelea na msako, tumekamata watu wengi sana na wengine utapofika wakati watawekwa wazi na vyombo vyetu lakini kuna hilo tatizo ni watanzania wenzetu wanaofanya haya mambo, ingawa wakati mwingine napata mashaka kwamba unawezaje kufanya hivi kwa nchi yako yaani unafanya ili iweje,” alisema.

Kadogosa alisema pamoja na mifumo iliyopo katika baadhi ya maeneo kama vile madaraja watalazimika kuwa na mfumo wa ulinzi katika maeneo yote ili kuepuka hasara inayoweza kutokana na wahujumu wa miradi, jambo ambalo linahitaji gharama kubwa kulitekeleza.

Alisema kuna ujenzi ambao unaendelea wa reli kati ya Makutupora na Tabora na Tabora kwenda Isaka pamoja na Isaka kwenda Mwanza ambao umekaribia asilimia 70 na kuwa wakati wowote upo uwezekano wa kusaini mkataba wa ujenzi kutoka Uvinza kwenda Msogati.

“Tunategemea kimkataba kuunganisha kutoka Makutupora mpaka Mwanza tutamaliza 2027 lakini kwa kipande cha kutoka Makutupora-Isaka, kwa kipande cha Isaka-Mwanza tunatarajia kumaliza mwakani kuelekea mwishoni mwa mwaka tutakuwa tumemaliza ujenzi, kutoka Tabora kuelekea Kigoma tunategemea kimkataba tutamaliza 2028,” alifafanua.