Mapitio muhimu kuhusu kodi ya mashirika

MFUMO wa kodi ya mashirika nchini ulioanzishwa kusaidia mapato ya umma na kuvutia uwekezaji wa biashara, unakutana na changamoto za ufanisi mdogo na ukosefu wa usawa unaokwamisha maendeleo ya taifa kiuchumi.

Tangu mwaka 1996, Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) imekuwa ikifanya maboresho kadhaa kuimarisha usimamizi wa kodi.

Hata hivyo, bado kuna mapengo makubwa katika ufanisi na utekelezaji wa sera. Kwa Tanzania, kiwango cha kodi kinachotumika kwa mashirika yote ya ndani ni asilimia 30 na hiki ndicho kinachotumika ulimwenguni kote kwa mashirika ya wakaazi.

Advertisement

Kiwango hiki kimekusudiwa kuleta uwiano kati ya kuvutia uwekezaji wa kigeni na kuzalisha mapato muhimu ya umma. Hata hivyo, kutokana na muundo wa uchumi wa Tanzania sekta isiyo rasmi inachangia takribani asilimia 47 ya pato la taifa, huku biashara ndogo na za kati (SMEs) zikiwa na nafasi muhimu.

Kiwango kimoja cha ushuru kinachotumika kwa wote, bila kujali ukubwa wa kipato au biashara kinaweza kisiwe rafiki zaidi kwa ukuaji wa uchumi. Kiwango cha kodi cha asilimia 30 kinaweza kuwa kikwazo kwa biashara ndogo na za kati (SMEs) na hata kuathiri vibaya shughuli za ndani za kiuchumi pamoja na ubunifu.

Sera na sheria zinazosimamia kodi ya mashirika Tanzania Mfumo wa kodi ya mashirika nchini unasimamiwa na sheria, sera na kanuni madhubuti zinazolenga kuhakikisha kuna utekelezaji wa sheria, ukusanyaji wa mapato na kuweka mazingira bora ya uwekezaji.

Msingi wake mkuu ni Sheria ya Kodi ya Mapato ya Mwaka 2004, inayoweka kiwango cha kawaida cha kodi cha asilimia 30 ikifafanua mapato yanayopaswa kutozwa kodi na kubainisha makatazo na misamaha katika biashara.

Biashara ndogo hunufaika na usimamizi wa kodi ya makadirio, huku sekta maalumu kama uchimbaji wa madini na mafuta zikifanya kazi chini ya masharti maalumu. Sheria ya Kodi ya Ongezeko la Thamani (VAT) ya Mwaka 2014 huathiri kodi ya mashirika kwa njia isiyo ya moja kwa moja kwa kudai biashara zote kuzingatia VAT, hivyo kuathiri mzigo wa kodi wa biashara.

Ili kuvutia uwekezaji, Sheria ya Uwekezaji ya Mwaka 1997 inatoa msamaha wa muda maalumu katika miradi inayolenga kuvutia wawekezaji, msamaha na viwango vya kodi vya upendeleo kwa sekta za kimkakati kwa maendeleo ya taifa, huku Sheria ya Uchimbaji wa Madini ya Mwaka 2010 (iliyorekebishwa Mwaka 2017) ikianzisha sera za kodi maalumu za sekta ili kuongeza uwazi na kuhakikisha kuna ushiriki sawa wa mapato.

Sheria za fedha zinazosasishwa kila mwaka huonesha vipaumbele vya serikali katika masuala ya fedha kwa kufanya maboresho katika sheria za kodi, kurekebisha viwango au kubadilisha motisha.

Aidha, Sheria ya Ubia baina ya Sekta ya Umma na Binafsi (PPP) ya Mwaka 2010 husaidia miradi ya miundombinu na nishati kupitia manufaa yatokanayo na kodi kwa mashirika yanayohusika katika miradi hii.

Usimamizi wa kodi umewekwa pamoja chini ya Sheria ya Utawala wa Kodi ya Mwaka 2015, inayowezesha Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) kutekeleza sheria, kusimamia usajili na kutatua migogoro. Kikanda, sera za kodi za Tanzania zinathiriwa na uanachama wake katika Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC) na Jumuiya ya Maendeleo ya Kusini mwa Afrika (SADC) zinazolenga kuoanisha sheria za kodi na kupunguza utozwaji kodi zaidi ya mara moja kati ya nchi wanachama.

Kwa pamoja, vyombo hivi vya sheria na sera hutoa mfumo wa kodi ya mashirika nchini unaolenga kuhakikisha kuna uwiano kati ya vipaumbele vya ndani na malengo ya kanda. Hata hivyo, ufanisi katika kufikia malengo ya uwekezaji hutegemea msimamo katika utekelezaji, ufanisi katika usimamizi na uwezo wa kuendana na mabadiliko ya hali ya kiuchumi. Uchambuzi wa takwimu Uchambuzi wa ukusanyaji wa kodi ya mashirika Tanzania Bara tangu mwaka 1996 hadi 2022 unaonesha mwelekeo mkubwa.

Uchambuzi wa mabadiliko ya kodi ya mashirika unaozingatia mfumuko wa bei unaonesha mwelekeo wa kupanda kama inavyooneshwa na mstari mwekundu kwenye chati. Mteremko chanya unaonesha kwamba ukusanyaji wa kodi ya mashirika umeongezeka katika kipindi hiki.

Thamani ya R mraba (‘R’-squared) takribani 0.828, inaonesha kuwa asilimia 82.8 ya tofauti katika ukusanyaji wa kodi ya mashirika kwa kuzingatia mfumuko wa bei, inatokana na mchakato wa muda, ikionesha uhusiano kati ya mwaka na mapato halisi ya kodi. Kuhusu mabadiliko, tofauti ya kawaida ya ukusanyaji wa kodi ya mashirika ni takribani 942,696.

Hii inaonesha mabadiliko makubwa ya kiasi kilichokusanywa kwa mwaka. Ulinganifu wa tofauti au mabadiliko ya thamani kwa 1.045 unabainisha kuwa, viwango vya tofauti ni karibu asilimia 104.5 ya wastani. Hii inaonesha kuwa kuna tofauti kubwa katika takwimu zilizokusanywa.

Hii inaonesha kuwa, ingawa mwelekeo wa jumla unakwenda juu, mapato ya kodi ya mwaka hadi mwaka yanakutana na mabadiliko makubwa yanayoweza kutokea kutokana na hali ya uchumi, faida ya mashirika au mabadiliko ya sera za kodi.

Kimsingi, matokeo haya yanaonesha ukuaji thabiti wa mapato ya kodi ya mashirika kwa wakati, ukiambatana na kiwango kikubwa cha mabadiliko kila mwaka. Hii ina maana kuwa, kwa mipango ya fedha na bajeti, serikali haiwezi kutegemea kikamilifu ukuaji thabiti wa mapato ya kodi ya mashirika. Ingawa mwelekeo wa muda mrefu ni wa kupanda, kutotabirika kwa kipindi kifupi kunaibua changamoto katika kupanga matumizi.

Huenda watunga sera wakahitaji kubaini njia za kudhibiti mapato ya kodi, kama vile kuongeza vyanzo vya kodi au kuanzisha mikakati ya kupunguza mabadiliko katika ukusanyaji wa kodi.

Uwiano wa kodi ya mashirika GNI Uchambuzi wa takwimu za kodi Tanzania Bara tangu 1996 hadi 2022, unatoa maelezo yanayovutia kuhusu uhusiano kati ya michango ya kodi ya mashirika na makusanyo ya jumla ya kodi.

Uwiano wa kodi ya mashirika kwa GNI unaooneshwa kwa mstari wa kijani ukionesha kushuka kwa kiwango sawa kwa miaka kadhaa kuanzia takribani asilimia 1.52 mwaka 1996, na kushuka kwa kiasi kikubwa hadi mwaka 2022.

Mstari wa dashi wa rangi ya chungwa unaonesha uwiano wa wastani wa asilimia 1.19 ukitumika kama kipimo cha kulinganisha. Mwenendo huu unaonesha kuwa, mapato ya mashirika kama sehemu ya pato la taifa yamekuwa yakipungua. Kwa upande mwingine, makusanyo jumla ya kodi (NET), yanayooneshwa na mstari wa buluu, yanaonesha mwelekeo thabiti wa kupanda unaodhihirisha kuwapo kwa jitihada za maboresho katika ukusanyaji wa kodi au ukuaji wa uchumi.

Kutenganishwa kati ya makusanyo ya kodi ya jumla yanayopanda na uwiano wa kodi ya mashirika kwa GNI unaoshuka kunaonesha mabadiliko katika muundo wa kodi, ambapo kodi nyingine, kama vile VAT au kodi ya mapato zina mchango mkubwa zaidi katika makusanyo ya jumla ya kodi. Maelezo katika miaka muhimu yanasisitiza ukubwa wa mabadiliko haya yakidhihirisha kuwa, ingawa uwezo wa serikali kukusanya kodi umeimarika, kodi ya mashirika imekuwa sehemu ndogo ya pato la taifa na tofauti hii inazua maswali muhimu ya kisera.

Ingawa makusanyo jumla ya kodi yanaongezeka, kushuka kwa mchango wa kodi ya mashirika kunaweza kuashiria kuwapo ufanisi mdogo, mabadiliko ya muundo wa uchumi, au utegemezi mkubwa katika vyanzo vingine vya kodi.

Watunga sera wanapaswa kuchunguza sababu za msingi, kama vile motisha za kodi, upungufu katika utekelezaji, au mabadiliko katika uchumi ili kuhakikisha msingi wa mapato ni imara na endelevu.

Uchambuzi huu unasisitiza haja ya kuoanisha kwa karibu zaidi, michango ya kodi ya mashirika na ukuaji wa uchumi. Mapitio ya sera za duniani duniani kote, viwango vya kodi ya mashirika hutofautiana na kuakisi vipaumbele.

tofauti vya kiuchumi kama inavyoonekana katika mgawanyo wa viwango vya kodi ya mashirika katika nchi 148, zinazowakilisha asilimia 76 ya mataifa 195 yaliyotambuliwa duniani.

Kiwango cha asilimia 20-30 ni cha kawaida kikihusisha nchi 70 kama Marekani, Ujerumani, China na nchi zinazoendelea kama Tanzania, Kenya na India. Kipengele hiki kinawakilisha uwiano kati ya kuvutia uwekezaji wa moja kwa moja wa kigeni (FDI) na kuzalisha kiwango cha kutosha cha mapato ya umma.

Wigo wa asilimia 0-10 wa nchi 13 pekee (asilimia tisa) unajumuisha maeneo ya kodi ya chini kama vile Bahamas, Visiwa vya Cayman na Hungaria vinavyotumia viwango vya kodi vya chini sana ili kujijengea nafasi ya kuwa kitovu cha fedha duniani.

Mara nyingi nchi hizi hutegemea vyanzo vingine vya mapato, kama vile utalii na huduma za fedha kufidia mapato ya kodi ya mashirika.

Kwa upande mwingine, wigo wa asilimia 30-40 unajumuisha nchi 19 (asilimia 13) zikiwamo Argentina, Brazil na Malta zinazotoa vipaumbele kuzalisha mapato kupitia viwango vya juu vya kodi. Hata hivyo, viwango hivi vinaweza kupunguza ushindani katika kuvutia uwekezaji wa kimataifa.

Kiwango cha asilimia 10-20 chenye nchi 32 (asilimia 22) kinaonesha uchumi wa nchi kama vile Ireland, Singapore, na Romania zinazotumia viwango vya chini vya kodi ya mashirika pamoja na motisha kwa sekta maalumu kuvutia FDI katika viwanda kama vile teknolojia na fedha.

Uchambuzi unabainisha mwelekeo wa kidunia kuelekea viwango vya kodi vya wastani, ambapo nchi nyingi zinajumuisha kipengele cha asilimia 10-30 na kuonesha umuhimu wa sera za kodi zilizozingatia uwiano kudumisha ustawi wa kifedha na ukuaji wa uchumi.

Nchi zisizo na kodi ya mashirika kama vile Bahrain na Bermuda mara nyingi hutegemea sekta kama utalii au rasilimali za asili. Matokeo haya yanasisitiza tofauti katika mikakati ya kodi ya mashirika huku mataifa yakifanya maboresho ya sera kadiri ya vipaumbele vya kiuchumi na kuwianisha ushindani na mahitaji ya mapato.

Uwiano wa mapato na FDI Uchambuzi unabainisha maoni muhimu kuhusu uhusiano kati ya viwango vya kodi ya mashirika na viwango vya ukuaji wa Pato la Taifa (GDP). Katika kundi la kodi la asilimia 0-10, nchi hupata kiwango cha juu cha ukuaji wa pato la taifa cha wastani cha asilimia 9.7 kinachoonesha uwezekano wa kuimarika kwa uchumi kutokana na kodi ndogo.

Hii inaweza kuakisi mazingira mazuri ya biashara, ongezeko la uwekezaji, au hali maalumu kama uchumi mdogo au maeneo ya kodi yanayochochea ukuaji mkubwa. Katika kundi la asilimia 10-20, kiwango cha ukuaji wa pato la taifa kinashuka kwa kiasi kikubwa hadi asilimia 4.37 kikidhihirisha kuwa, ingawa viwango vya kodi vya wastani bado vinasaidia ukuaji, pia vinaweza kuleta vizuizi vya kiuchumi vikilinganishwa na viwango vya chini.

Cha kushangaza, kundi la asilimia 20-30 kinashuhudia ongezeko kidogo kwa ukuaji cha pato la taifa la wastani wa asilimia 5.46.

Hii inaashiria kuwa, ingawa viwango vya juu vya kodi vinaweza kuleta mizigo ya ziada, sababu nyingine kama uthabiti wa uchumi au matumizi sahihi ya serikali katika mapato ya kodi yanaweza kupunguza vikwazo vya ukuaji. Katika kundi la kodi la asilimia 30-40, wastani wa ukuaji wa pato la taifa ni asilimia 5.56 ambacho ni juu kidogo kuliko kundi la asilimia 20-30.

Matokeo haya yanaonesha kuwa, kwa viwango vya juu vya kodi, uchumi unaweza kutulia au hata kuimarika kidogo kama kodi hizo ni sehemu ya sera ya fedha au kama zitaunganishwa na sababu nyingine zinazosaidia ukuaji.

Hitimisho Ingawa kiwango cha kodi ya mashirika cha asilimia 30 nchini kinalenga kuweka uwiano kati ya uwekezaji na uzalishaji wa mapato, huenda kisishughulikie kikamilifu changamoto za uchumi, kwa kuwa uhusiano usio wa moja kwa moja kati ya viwango vya kodi na ukuaji wa pato la taifa unaonesha hitaji la sera za kimkakati zinazosaidia ukuaji huku zikihakikisha kuna ustahimilivu wa kifedha.

Uchambuzi unadhihirisha kuwa, ingawa viwango vya chini vya kodi mara nyingi husababisha ukuaji mkubwa wa uchumi, viwango vya wastani hadi vya juu vina matokeo mchanganyiko yanayoweza kuathiriwa na sababu za uchumi mpana na muundo wa uchumi. Matokeo haya yanaonesha umuhimu wa kubuni sera za kodi za kimkakati ili kuweka uwiano sawia unaolenga kukuza ukuaji wa uchumi na kuzalisha mapato endelevu.

Tanzania inapaswa kuangalia upya sera zake za kodi ya mashirika kwa kuweka msisitizo katika kuzingatia utayari katika mabadiliko, usawa na msukumo wenye ufanisi ili kujenga uchumi stahimilivu unaochochea ukuaji endelevu huku ukipokea mifumo ya aina mbalimbali kuboresha usawa na ujumuishaji katika sekta na viwango vya biashara.