Mapya yaibuka ajali iliyoua 20 Tanga

Yadaiwa marehemu hakutaka kuzikwa Rombo

NDUGU wa marehemu Athanas Mrema aliyekuwa akisafirishwa katika gari lililopata ajali na kuua watu 20 Korogwe mkoani Tanga, wamedai kuwa ndugu yao hakutaka kwenda kuzikwa Rombo mkoani Kilimanjaro.

Inadaiwa kuwa Mrema alitengana na mkewe anayeishi Rombo kwa zaidi ya miaka 20 na aliomba akifariki dunia asipelekwe kuzikwa huko.

Ndugu wa Mrema, Aqueline Massawe (72) alidai ajali iliyosababisha vifo vya watu 20 ni ishara kwamba familia inahitaji maombi na mila kuvunja kiapo cha ndugu yake.

Massawe alisema hayo alipozungumza na HabariLEO katika eneo la Hospitali ya Huruma wilayani Rombo wakati wa kuaga miili ya watu 12 kati ya 20 waliokufa kwenye ajali hiyo Februari mwaka huu saa 4:30 usiku katika eneo la Magila Gereza.

Ajali hiyo ilitokea wakati lori aina ya Mitsubishi Fuso lenye namba za usajili T 673 CUC lilipogongana uso kwa uso na Toyota Coaster lenye namba za usajili T 863 DXN ikiwa imebeba mwili wa marehemu na waombolezaji wakienda kuzika Moshi mkoani Kilimanjaro.

Wanaukoo waliokufa katika ajali hiyo ni Doris Mrema, Tonny Mrema, Augustina Mrema, Evelina Mrema, Kennedy Mrema, Godfrey Mrema, Zawadi Mrema, Elizabeth Mrema, Julieth Mrema, Cosmas Mrema na Rajab Mrema.

Ndugu mwingine wa Mrema, Thomas Masheli (74) aliyejitambulisha kuwa ni shemeji wa familia ya marehemu alithibitisha kufahamu mgogoro wa kifamilia baina ya Mrema na mkewe kwa zaidi ya miaka 15 iliyopita.

“Enzi za uhai wa Athanas alikataa kurejeshwa Rombo na akaongeza kuwa watakaolazimisha ataondoka nao…huu usemi tulikua tukiusikia lakini hakuna aliyetilia maanani, sasa imeleta maafa, ukoo unatakiwa uvunje kiapo hiki,” alisema.

Athanas alizikwa nyumbani kwake Kitongoji cha Kitunguu Kata ya Kelamfua Mokala pamoja na mtoto wake mmoja na mjukuu.

Mtoto wake alitajwa kuwa ni Augustina Mrema na Tonny Mrema aliyetajwa kama mjukuu ambao walikufa kwenye ajali hiyo.

Wengine waliozikwa katika eneo moja katika Kitongoji cha Kitunguu ni Godfrey Mrema, Kennedy Mrema na Nestor Kiwango aliyekuwa Maktaba katika Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM) alizikwa Kijiji cha Shimbi.

Miili ya watu wengine watatu kati ya sita itazikwa kuanzia leo katika eneo la Mengwe wilayani Rombo ambalo atazikwa Avelina Mrema na mumewe Elimian Lyakurwa na mwili mwingine utazikwa eneo la Kilema.

Miili ya watu wengine watatu itazikwa wilayani humo kulingana na taratibu za familia husika.

Wakati wa ibada ya kuaga miili jana Mkuu wa Mkoa wa Kilimanjaro, Nurdin Babu aliomba viongozi wa dini katika makanisa na misikiti wafanye maombi kupunguza athari katika ajali na pia Jeshi la Polisi lisimamie madereva waheshimu alama za usalama barabarani.

Awali Askofu wa Jimbo Katoliki la Moshi, Ludovick Minde alitoa mwito kwa watu waepuke kusafiri katika chombo kimoja cha usafiri ili kuepuka maafa yanayoweza kujitokeza.

Pia Askofu Minde aliomba jamii ijifunze kuacha kusafiri usiku ili kupunguza athari zinazoweza kuepukika.

Katika ibada hiyo, Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Profesa Adolf Mkenda

aliomba jamii ipunguze utamaduni wa kutumia chombo kimoja cha usafiri ili kupunguza ukubwa wa athari zitakazojitokeza.

Wakati huo huo serikali imetoa zaidi ya Sh milioni nne zikiwa ni ubani kwa familia za watu 20 wakiwamo wana ukoo 13 waliopoteza maisha katika ajali ya gari iliyotokea Korogwe mkoani Tanga.

Mkuu wa Mkoa wa Tanga, Omari Mgumba alisema mjini Tanga jana kuwa majeruhi saba kati ya tisa wanaendelea kupata tiba katika Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Tanga, Bombo.

Majeruhi wawili waliruhusiwa jana.

Mgumba alisema hayo wakati wa majumuisho ya ziara ya siku sita ya Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar, Hammed Suleimani Abdulla ambaye pia ni mlezi wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Mkoa wa Tanga.

“Niwaambie tu wananchi wa Tanga na serikali kwa ujumla kuwa shukrani za pekee ziende kwa Rais Samia Suluhu Hassan kwa moyo wake wa huruma kwa maelekezo ya serikali yake kugharamikia mazishi, majeneza yote ni gharama za serikali na imetoa ubani wa zaidi ya shilingi milioni nne,” alisema Mgumba.

Imeandikwa na Nakajumo James (Rombo) na Amina Omari (Tanga).

Habari Zifananazo

Back to top button