WASHINGTON DC : SERIKALI ya Marekani imeiwekea Iran vikwazo vipya, siku chache tu baada ya Rais Donald Trump kutangaza mpango wa kuanzisha mazungumzo kuhusu mradi wa nyuklia wa taifa hilo la Mashariki ya Kati.
Hatua hiyo inaelezwa kuwa ni sehemu ya mkakati wa kuishinikiza Iran ikubali kushiriki mazungumzo hayo yanayotarajiwa kufanyika Jumamosi hii nchini Oman. Trump ameendelea kusisitiza kuwa kama Iran haitasitisha shughuli zake za kinyuklia, basi Marekani haijasita kutumia nguvu za kijeshi. Aidha, Israel inatajwa kuwa na nafasi ya kipekee katika mchakato huo.
Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran amethibitisha uwepo wa mkutano huo utakaofanyika Aprili 12, lakini akasisitiza kuwa hautakuwa wa ana kwa ana. Kwa miaka mingi, Marekani na washirika wake wamekuwa wakipinga juhudi za Iran za kuendeleza uwezo wa kinyuklia, wakisisitiza kuwa hatua hiyo ni tishio kwa usalama wa kimataifa.
Tangu makubaliano ya mwaka 2015 yaliyoanzishwa na utawala wa Rais Barack Obama, ambapo Iran ilikubali kupunguza shughuli za nyuklia na kuruhusu ukaguzi wa kimataifa, hali imebadilika. Trump alijiondoa kwenye makubaliano hayo mwaka 2016 na tangu wakati huo, Iran imekiuka masharti kadhaa, ikiwemo kuongeza uzalishaji wa urani.
SOMA: Marekani , Iran kujadili mpango wa nyuklia
Israel imeendelea kuonyesha msimamo mkali dhidi ya Iran, ambapo mwaka jana iliripotiwa kushambulia kituo cha nyuklia cha taifa hilo, ikidai kulipiza kisasi kutokana na mashambulizi ya makombora kutoka Tehran. Mvutano huu unachochewa pia na historia ndefu ya uhasama kati ya mataifa hayo, tangu mwaka 1979, ambapo ubalozi wa Marekani mjini Tehran ulivamiwa na maafisa kushikiliwa mateka. Marekani sasa inaongoza kwa kuiwekea Iran vikwazo vingi zaidi kuliko nchi nyingine yoyote duniani.