MAKAMU wa Rais wa Marekani, JD Vance ameahidi kuwa Washington inalenga kufanikisha ‘amani ya kudumu’ katika mzozo unaoendelea kati ya Urusi na Ukraine.
Kauli ya Vance inalenga kupunguza wasiwasi miongoni mwa washirika wa Ukraine kuhusu mipango ya Marekani ya kumaliza vita ambavyo vimekuwa vikiendelea kwa muda mrefu.
Vance alitoa ahadi hiyo wakati wa mazungumzo yake ya kwanza na Rais Volodymyr Zelensky wa Ukraine, yaliyofanyika pembezoni mwa Mkutano wa Kimataifa wa Usalama huko Munich.
Soma zaidi: Ukraine yadai mapema kushiriki mkutano wa amani
Alisema kuwa Marekani imedhamiria kufikia amani ya kudumu itakayozuia mizozo zaidi katika eneo la Mashariki mwa Ulaya kwa miaka ijayo.
Kauli ya Vance ililenga kuondoa hofu inayozidi kutanda miongoni mwa washirika wa Ukraine hasa Ulaya, kufuatia matamshi yaliyotolewa na Rais Donald, Trump alitangaza kuwa mazungumzo ya kumaliza vita vya Ukraine yanaweza kuanza hivi karibuni baada ya kufanya mazungumzo na Rais Vladimir Putin wa Urusi na Rais Zelensky.
Wengi wameshtushwa na wazo kwamba Marekani inaweza kufikia makubaliano na Urusi bila kuizingatia kikamilifu Ukraine au kuihakikishia usalama wa kudumu.
Soma zaidi: Nitamaliza vita vya Urusi na Ukraine – Trump
Hofu hii imekuwa ikiendelea tangu matamshi hayo ya Trump, na washirika wa Ukraine wakiwa na wasiwasi kwamba Marekani itafikia muafaka na Urusi bila kujali usalama wa Ukraine
Hata hivyo, katika mazungumzo yake ya Munich, Rais Zelensky alisisitiza kuwa yeye yuko tayari kushirikiana na Marekani katika juhudi za kumaliza vita, akisisitiza kuwa amani ya kudumu na usalama wa nchi yake ni msingi mkuu wa mazungumzo yoyote.