“Marufuku ushuru mazao yanayouzwa kwa NFRA”

RUKWA: Serikali mkoani Rukwa imewataka wakurugenzi wa halmashauri mkoani humo kutotoza ushuru wa mazao yanayouzwa na Vyama vya Ushirika kwa Wakala wa Taifa wa Hifadhi ya Chakula (NFRA).

Aidha, badala yake ushuru huo ukusanywe na NFRA kwa niaba ya halmashauri.

Agizo hilo limetolewa na Mkuu wa Wilaya ya Kalambo, Dk Lazaro Komba alipomwakilisha Mkuu wa Mkoa wa Rukwa Charles Makongoro Nyerere katika Mkutano wa Nane wa Jukwaa la Vyama vya Ushirika uliofanyika katika ukumbi wa mikutano wa Moravian, Sumbawanga.

Akizungumza mbele ya viongozi wa vyama  hivyo, wadau wa kilimo na maofisa wa serikali, Dk Komba amesema kuwa hatua hiyo inalenga kuhamasisha na kuimarisha ushirika Rukwa ikiwa ni pamoja na kupunguza usumbufu kwa wakulima walio wanachama wa vyama hivyo.

Dk Komba amesema kuwa serikali  inahimiza kukuzwa kwa ushirika na hivyo kuwataka viongozi kujenga mazingira rafiki ya kukuza ushirika kwa kuzingatia sheria na taratibu zilizopo.

Pamoja na maelekezo hayo ya Serikali ya Mkoa, Dk Komba ameeleza juu ya utayari wa serikali kusimamia haki na maslahi ya wananchama wa vyama vya ushirika ili kuongeza tija katika kilimo, mifugo na uvuvi.

Kwa upande wao, baadhi ya viongozi wa vyama vya ushirika wameipongeza Serikali kwa juhudi za kuhamasisha na kuulinda ushirika jambo linaloongeza nafuu na tija kwa wakulima.

Habari Zifananazo

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Back to top button