IMEELEZWA kuwa mashamba yasiyoendelezwa yamekua chanzo kikubwa cha migogoro ya ardhi wilayani Kakonko mkoani Kigoma ikiwemo mashamba ya kurithi ambayo hayana nyaraka zozote za umiliki
Ofisa Ardhi wa Halmashauri ya Wilaya Kakonko, Gideon Kimaro amesema hayo wakati wa muendelezo wa Kampeni ya Msaada wa Kisheria ya Mama Samia inayoendelea na mikutano mbalimbali ya wananchi wilayani humo.
Ofisa Ardhi Halmashauri ya Wilaya Kakonko, Gideon Kimaro akitoa elimu kuhusu sheria ya ardhi na umiliki ardhi kihalali kwa mujibu wa sheria kupitia Kampeni ya Msaada wa Sheria ya Mama Samia
Akieleza kuhusu hilo ofisa ardhi huyo amesema serikali kupitia serikali za vijiji imekuwa ikiweka mipango ya matumizi bora ya ardhi ili kuwezesha kuondokana na migogoro ili kila shughuli ifanyike maeneo yaliyoanishwa na wananchi wanapaswa kutumia ardhi hiyo kulingana na mipango iliyowekwa.
Akizungumza katika mikutano hiyo Ofisa Maendeleo ya Jamii wa Halmashauri ya Wilaya Kakonko, Nicholous Muhebera amesema migogoro mingi vijijini inasababishwa na ukiukwaji wa sheria za ardhi namba 8 na namba 5 za mwaka 1999 ambazo zinataka wanaotaka kumiliki ardhi kufuata sheria hizo na kwamba hiyo ndiyo njia pekee ambayo itamuwezesha mwananchi kumiliki ardhi kihalali na kutoingia kwenye mgogoro na serikali au na mwananchi mwenzake.
Ofisa Maendeleo ya Jamii Halmashauri ya Wilaya Kakonko, Nicholous Muhebera akizungumza katika mfukulizo wa mikutano ya Kampeni ya Msaada wa Sheria ya Mama Samia Wilaya Kakonko
Kwa upande wake mratibu wa kampeni hiyo, Jackline Kulwa amesema kuwa katika kampeni hiyo ya siku 10 wilayaani Kakonko wanatarajia kufika kwenye kata 10 na kuvifikia vijiji 30 ambapo watatoa msaada wa kisheria, miongozo na kusikiliza kero za wananchi ili ziweze kufanyiwa kazi kulingana na sheria na taratibu za nchi.
Mratibu wa Kampeni ya Msaada wa Sheria ya Mama Samia Jackline Kulwa (akizungumza) na wananchi wa kijiji cha Gwarama halmashauri ya Wilaya Kakonko katika muendelezo wa kampeni hizo.
Kulwa amesema kuwa kampeni hiyo imefika hadi vijijini vya mbali kabisa mbali na makao makuu ya wilaya au kata ili kuwezesha kusikilizwa kwa kero za wananchi zilizosababisha kukosa haki zao mbalimbali hivyo wote watakaojitokeza kesi zao zitasikilizwa na kutafutiwa ufumbuzi kwenye mamlaka zinazohusika na malalamiko yaliyotolewa.