Tamasha la Taarabu kufanyika Agosti 28

DAR ES SALAAM: MSEMAJI wa muziki wa taarabu utakaoshirikisha mastaa na wakongwe wa muziki huo nchini, utakaofanyika Agosti 28 mwaka huu katika Viwanja vya Posta, Kijitonyama, unatarajiwa kuwa na mgeni rasmi Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Albert Chalamila.
Akizungumza na waandishi wa habari, Mboni Masimba, Mkurugenzi wa Kampuni ya Chocolate Princess Limited, wakiandaa tamasha hilo, alisema mkesha huo ni bure na umeandaliwa mahsusi kwa wadau wa Chama cha Mapinduzi (CCM), ukiwa na kauli mbiu “Wanamwambao tunatamba na Mama”.
Mboni alisema tamasha hilo limepangwa karibu na kampeni za kisiasa ili kutoa hamasa kwa wapenzi wa taarabu kushiriki burudani na kuunga mkono Rais Samia Suluhu Hassan. “Tutaanza saa 10 jioni hadi majogoo, kisha tutaelekea kwenye uzinduzi wa kampeni,” alisema.
Tamasha hilo linatarajiwa kuvuta mashabiki lukuki kutokana na orodha ya wakongwe wa taarabu wakiwemo Khadija Kopa, East Afrika Melody, Sabah Muchacho, Khadija Yusuf, Isha Ramadhani ‘Isha Mashauzi’, Mwanahawa Ally, Mzee Yusuf, Zanzibar One, na Leila Rashid.
Kwa upande wake, Mzee Yusuf alisema taarabu ni muziki unaoibeba Tanzania kimataifa. “Ukienda duniani kote ukitaja taarabu, watu wanaielekeza Tanzania. Muziki huu unaweza kuchezwa na rika zote bila kubagua. Tamasha hili limekuja kwa wakati muafaka,” alisema.
Pia, Palina Ninje, Mwenyekiti wa Umoja wa Wanawake Wachimbaji Madini Tanzania, alisema kushiriki mkesha huo kumemgusua kwani unaleta sura mpya ya siasa na burudani. “Siasa si mikutano pekee. Kupitia muziki wa taarabu, vijana wameajiriwa na vipaji vinajulikana. Tarehe 28 tutamsindikiza Rais Samia, kwa mara ya kwanza nchi yetu ikiingia kwenye historia kubwa ya kisiasa,” alisema.
Palina aliwataka wanawake wote nchini, bila kujali vyama vyao, kujitokeza kumsapoti Rais Samia kupitia tamasha hili na kwenye uzinduzi wa kampeni. SOMA: Mzee yusuph ajivunia muziki wa taarabu



