Matarajio ya wengi ni mafanikio CHAN, AFCON

MWANAHABARI na mtu wa sheria, Profesa Palamagamba Kabudi ameelekezwa na Rais Samia Suluhu Hassan kusimamia maandalizi ya mashindano ya Mataifa ya Afrika kwa wachezaji wa ndani (CHAN) na yale ya AFCON.

Tanzania kwa kushirikiana na nchi jirani za Uganda na Kenya zitaandaa CHAN mwakani na AFCON mwaka 2027.

Rais Samia akizungumza baada ya kumuapisha Profesa Kabudi kuwa Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Ikulu Ndogo ya Tunguu, Unguja, alisema pamoja na kupelekwa kusimamia sekta ya habari ambayo ameihamishia huko, amemtaka kumpatia Naibu Waziri wake Hamisi Mwinjuma msukumo wa kusimamia vyema michezo, sanaa na utamaduni ili matarajio ya taifa yafanikiwe.

Advertisement

Tanzania imejenga matumaini makubwa kuvuna fursa za kufanikisha mashindano ya Kombe la Mataifa Afrika kwa wachezaji wa ndani yatakayofanyika Februari Mosi hadi 28, mwakani na AFCON itafanyika mwaka 2027 ambapo Tanzania, Kenya na Uganda zinashirikiana kuandaa.

Profesa Kabudi ambaye anatoka Wizara ya Katiba na Sheria amechukua nafasi ya Dk Damas Ndumbaro ambaye sasa amepelekwa kuwa Waziri wa Katiba na Sheria, ana kazi kubwa kuhakikisha matumaini hayo yanafikiwa.

Uamuzi wa Tanzania kuandaa mashindano ya CHAN na AFCON ni fursa kubwa kwa Tanzania kuweka historia mpya katika ulimwengu wa soka na hiyo inawezekana kwa kuhakikisha hadidu za rejea za kufanikisha michuano hiyo,
ikiwamo viwanja vya mazoezi na kuchezea vinakamilika kabla ya muda uliowekwa.

Tayari timu ya watathmini kutoka Shirikisho la Soka Afrika (CAF) imeshatembelea nchini kuona maendeleo na kwa mujibu wa serikali tupo ndani ya muda, hivyo Rais Samia kwa kutoa angalizo hilo hataki kutokee sintofahamu katika kitu ambacho tayari kinakodolewa macho na Watanzania ambao upendo wao kwa soka si wa kawaida.

Kwa kuwa michuano ya CHAN itaanza mwakani, ni dhahiri kwamba siku zinahesabika. Kwa kufanikiwa  kukamilisha kwa wakati na hivyo kuanza hatua nyingine ya maandalizi, mafanikio yake yataitambulisha Tanzania
kama taifa lenye uwezo wa kuandaa matukio makubwa ya kimataifa.

Pamoja na kuiandaa Taifa Stars kufanya vyema katika michuano hiyo, kuna timu 24 zitakazoshiriki fainali za Mataifa ya Afrika 2025 na hivyo ni lazima masuala yote katika mnyororo wa michuano hiyo, ikiwamo viwanja na
huduma nyingine viwe katika hali inayotakiwa kwa mujibu wa kanuni na taratibu.

Tangu Septemba mwaka huu, Serikali ya Tanzania imekuwa ikionekana kujiandaa kwa vitendo kwa kujenga viwanja vipya, kukarabati vilivyopo hususan viwanja ambavyo vitatumika kwa mazoezi.

Wakati Rais Samia anaagiza kuhusu CHAN na AFCON, mamlaka za kiufundi, likiwamo Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) wanatakiwa kuendelea kupambana kuisuka timu ya taifa ili juhudi za serikali kufanikisha CHAN ziwe ni ushindi mkubwa kwa Taifa.

Mashindano ya CHAN ambayo ni mashindano ya kipekee kwa kuwa yanawapa wachezaji wanaocheza katika ligi za ndani za nchi zao nafasi ya kuwakilisha mataifa yao, yalianzishwa mwaka 2009 na yamekuwa yakifanyika kila baada ya miaka miwili.

Lengo kuu la mashindano haya ni kukuza soka la ndani na kutoa nafasi kwa vipaji vipya kuonekana.

Wakati umebaki mdogo, hivyo agizo la Rais Samia la kumtaka Profesa Kabudi kuhakikisha mambo yanaenda sawa yapo katika dhamira aliyonayo ya kuhakikisha Tanzania inanufaika na rasilimali zake na pia kuonesha uwezo wa kuitisha mashindano makubwa yatajayochangia kukua kwa soka na pia, uchumi wa nchi kwa kuongeza idadi ya watalii.

Pia, sekta mbalimbali za uchumi zitafaidika na mashindano haya, ikiwa ni pamoja na sekta ya hoteli, usafiri na
chakula. Serikali kwa kuthamini mahitaji ya kitaifa katika uchumi pia, inatumia njia ya kuwa mgeni kama fursa ya
kuboresha miundombinu ya michezo, ambayo itakuwa na manufaa kwa vizazi vijavyo.

Mashindano haya yatakuwa na mchango mkubwa katika kuinua hadhi ya soka la Tanzania na Afrika hivyo agizo la Rais Samia kwa maneno mengine ni kwamba, hakuna kubweteka, bali ni mapambano mpaka kieleweke.

Sio Profesa Kabudi pekee aliyeagizwa lakini kupitia yeye kuna mambo mengi yanatakiwa kufanyika ili kuhakikisha
maandalizi yanafanyika kwa mafanikio na hili Rais Samia anajua kuwa Profesa Kabudi anaweza kulikamilisha, hivyo
dhamana mabegani mwake ni kubwa.

Serikali imewekeza katika ujenzi na ukarabati wa viwanja vya michezo, hoteli na miundombinu mingine muhimu, hivyo Profesa Kabudi anatarajiwa kutumia uzoefu wake kuimarisha ushirikiano na sekta binafsi, mashirika ya
kimataifa na wadau wengine katika kufanikisha kuandaa mashindano haya.

Novemba Mosi, mwaka huu ilielezwa na Katibu Mkuu wa Wizara ya Utamaduni, Sanaa na Michezo, (kabla
haijaunganishwa na Habari), Gerson Msigwa kwamba Rais Samia ametoa Sh bilioni nane kwa ajili ya ujenzi na
ukarabati wa viwanja vya mazoezi vitavyotumika katika michuano ya CHAN 2025 na AFCON 2027.

Alisema hayo wakati akisaini mkataba wa ujenzi na Suma JKT kwa ajili ya ujenzi na ukatarabati wa viwanja vitano ambavyo ni Meja Jenerali Isamuhyo, Shule ya Sheria na ujenzi wa viwanja vipya Leaders, Farasi, Tirdo na Gymkhana.

Alisema ujenzi huo utahusisha uwekaji wa taa, majukwaa yatayochukua watu 2,000 katika viwanja vipya, njia za kupitisha maji na kupanda nyasi halisi ili kuendana na viwango vya CAF na vilitarajiwa kukamilika katika kipindi cha siku 120, sawa na miezi mitatu.

CAF wamepita na kutoa maelekezo na sasa ni kazi ya Profesa Kabudi kuuona mchakato mzima wa uboreshaji na ujenzi wa viwanja unakamilika hata kama ikibidi kwenda huko kila siku.

Mwanahabari Profesa Kabudi tunaamini ataangalia pamoja na CHAN, CAF itafanya ukaguzi wa viwanja na maandalizi ya AFCON 2027, Desemba mwaka 2025 ina maana Afrika Mashariki ina miaka miwili tu kuwa tayari kuandaa mashindano hayo makubwa barani.

Mtangulizi wake, Dk Ndumbaro akiwa Ivory Coast alisema, “Kwetu sisi huo muda unatosha, sehemu nyingi  hatujengi viwanja vipya, tutaboresha vilivyopo,” hivyo ni kazi ya Kabudi kuhakikisha tamko hilo linakamilika,
kwani ni tamko la serikali.

Pamoja na miundombinu, ni lazima Profesa Kabudi aunganishe wizara za kisekta ili kuhakikisha kwamba ‘Mauzo ya Mashindano’ yanafanikiwa ikiwa ni sehemu ya sababu ya kutaka kuandaa mashindano hayo.

Dk Ndumbaro alisikika Ivory Coast akisema kuwa, “Tunataka tuweke alama kubwa Afrika ili wadau wa soka waseme hawakufanya kosa kuleta AFCON ukanda wetu,” na sasa ni kazi ya Profesa Kabudi kuikamilisha.