MWAKA 2024 unaisha na sasa unaingia mwaka 2025, yapo matukio makubwa ambayo hayawezi kusahaulika kwa Watanzania likiwemo linalohusu Shirika la Afya Duniani (WHO) Kanda ya Afrika.
Ndiyo haliwezi kusahaulika kwa sababu lilitupa sana furaha Watanzania, tukapongezana, lakini mwishoni mwa mwaka 2024 likatuhuzunisha, tumelia nab ado tunalia, tumepigwa butwaa nini kimetokea. Ila hatutakiwi kukufuru badala yake tuseme kazi ya Mwenyezi Mungu haina makosa.
Tanzania ilipata heshima kubwa kwa mara ya kwanza kushiriki katika kinyang’anyiro cha kugombea nafasi ya Mkurugenzi wa WHO Kanda ya Afrika, pale Mbunge wa Kigamboni, Dk. Faustine Ndugulile, mtaalamu wa afya ya umma, alipoteuliwa kuwania nafasi hiyo akiwa miongoni mwa wagombea watano kutoka nchi mbalimbali Afrika.
Alikuwa akigombea nafasi ya kuongoza kanda hiyo, iliyoachwa wazi na Dk. Matshidiso Moeti.
Dk. Ndugulile aliwashinda wagombea kutoka nchi za Niger, Rwanda, Ivory Coast na Senegal.
“Nina dhamira thabiti ya kuendeleza afya na ustawi wa watu Afrika,” alisema Dk. Ndugulile katika hotuba yake ya kuchaguliwa, ambapo Rais wa Tanzania Dk.Samia Suluhu Hassan alimpongeza Dk. Ndugulile akisema kuwa ni fahari kwa Tanzania na bara zima la Afrika.
Wasifu wa Dk. Ndugulile
Dk. Ndugulile alikuwa daktari na mtaalamu wa afya, na pia alihusishwa na utawala wa afya nchini Tanzania, akiwa Mwenyekiti wa Kamati ya Bunge ya Afya na Makamu Mwenyekiti wa Umoja wa Mabunge ya Kimataifa.
Aliwahi pia kuwa Naibu Waziri wa Afya na Waziri wa Mawasiliano na Teknolojia ya Habari. Ndugulile alikuwa na historia ndefu ya kufanya kazi na taasisi za kimataifa kama CDC na akiwa na jukumu muhimu katika huduma za afya nchini Tanzania.
Kifo cha Dk. Ndugulile na msiba wa Taifa
Tanzania ilishtushwa na taarifa ya kifo cha Dk. Faustine Ndugulile, kilichotokea Novemba 27, 2024, wakati akiendelea na matibabu nchini India.
Taarifa ya msiba ilitangazwa na Spika wa Bunge, Dk. Tulia Ackson ilisema: “Nimepokea kwa masikitiko makubwa taarifa ya kifo cha Mbunge wa kigamboni na Mkurugenzi Mteule wa Shirika la Afya Duniani (WHO) Kanda ya Afrika, Dk. Faustine Ndugulile kwa niaba ya wabunge natoa pole kwa familia wakazi wa Kigamboni na Watanzania wote.”
Rais Samia alieleza masikitiko yake kwa msiba huo: “Nimepokea kwa masikitiko taarifa ya kifo cha Dk. Faustine Ndugulile, mbunge wa Kigamboni na Mkurugenzi mteule wa Shirika la Afya Duniani (WHO), Kanda ya Afrika, kilichotokea usiku wa kuamkia leo Novemba 27, 2024”.
Mkurugenzi Mkuu wa WHO, Dk. Tedros Adhanom Ghebreyesus, pia alieleza huzuni yake.
“Nimeshtushwa na kusikitishwa saana na taarifa nilizopokea za kifo cha ghafla cha Dk. Faustine Ndugulile ambaye alikuwa Mkurugenzi mteule wa Kanda ya WHO Afrika.”
Kuaga mwili na mazishi
Mwili wa Dk. Ndugulile ulirejeshwa nchini Tanzania Novemba 29, 2024, na kupokelewa na viongozi wa kitaifa na waombolezaji.
Desemba 3, 2024, Dk. Ndugulile alizikwa katika makaburi ya Mwongozo, Kigamboni. Shughuli ya mazishi ilihudhuriwa na viongozi wakuu, ikiwa ni pamoja na Waziri Mkuu Kassim Majaliwa, na viongozi wa kitaifa na kimataifa.
Dk. Ndugulile ameacha kumbukumbu kubwa kwa Tanzania, akiacha urithi wa utumishi na uongozi kwa kizazi cha sasa na kijacho. SOMA: Ndugulile afariki dunia akiwa na miaka 55
Tanzania itaendelea kumkumbuka kwa mchango wake katika maendeleo ya afya na ustawi wa jamii. Hakika kwa Ndugulile tulifurahi, lakini tukalia.