Matukio ya unyanyasaji 303 yaripotiwa ndani ya miezi tisa Morogoro

JUMLA ya matukio 303 ya vitendo vya ukatili kwa wanawake na watoto wakiwemo ya ubakaji yameripotiwa katika madawati ya jinsia na watoto ya Polisi mkoani Morogoro katika kipindi cha kuanzia Januari hadi Novemba mwaka huu (2022).

Katibu Tawala wa Mkoa huo, Dk Mussa Ali Mussa amesema hayo Desemba 8, 2022 wakati akitoa tamko la serikali ya mkoa kuhusu siku 16 za kupinga ukatili wa kijinsia kwa watoto na wanawake .

Kauli mbiu ya mwaka huu imebeba ukumbe : “ Kila uhai una thamani , tokomeza mauaji na ukatili dhidi ya wanawake na watoto “ .

Dk Mussa amesema kuwa, matukio hayo yamepungua kidogo ikilinganishwa na ya mwaka 2021 yaliyofikia 347.

Amesema matukio yaliyoongoza kati ya matukio 303 yaliyoripotiwa kwa mwaka huu, 56 ni ya ubakaji , 50 ulawiti na 38 mimba kwa wanafunzi .

Dk Mussa ametaja mengine na idadi yake katika mabano ni kumzorotesha mwanafunzi masomo yake ( utoro) (38) , shambulio la aibu (24) , kutorosha wanafunzi ( 11), kijaribu kubaka (14), kujeruhi (18), wizi wa mtoto( 1), shambulio la kawaida (26), shambulio la kudhuru mwili (10) na kufanya mapenzi na wanafunzi ni (7).

Amesema kati ya matukio hayo , 161 yamefikishwa mahakamani wakati 35 yametolewa hukumu na mengine 119 yapo katika uchunguzi na matukio 26 yamefutwa.

“ Matukio yote haya hasa ya kingono yamefanyika kwa kiasi kikubwa wa watoto na wanawake “ amesema Dk Mussa

Amesema serikali ya mkoa inaendelea kutekeleza afua mbalimbali kupambana na vitendo vya ukatili wa kijinsia kwa kuhuisha na kuratibu kamati za ulinzi wa wanawake na watoto katika ngazi zote kuanzia mkoa , halmashauri , kata na vijiji.

Dk Mussa amesema kuwa vitendo vya ukatili havikubaliki ,na wale ambao watabainika kufanya vitendo hivyo watachukuliwa hatua kali za kisheria.

Habari Zifananazo

1 Comment
Oldest
Newest Most Voted
Inline Feedbacks
View all comments
Back to top button