Matumizi ya chanjo yaongezeka Tanzania

TABORA : WAZIRI wa Afya, Jenista Mhagama, amesema kiwango cha uchanjaji kitaifa kwa miaka mitano mfululizo kimebakia zaidi ya asilimia 90, hatua inayoiweka Tanzania miongoni mwa nchi zinazofanya vizuri katika utoaji wa huduma za chanjo duniani.
Waziri Mhagama alitoa kauli hiyo mkoani Tabora wakati wa uzinduzi wa Maadhimisho ya Wiki ya Chanjo Kitaifa yenye kauli mbiu inasema, “ Chanjo ni kinga,tuungane kuwezesha walengwa wote wapate chanjo.”
Amesisitiza kuwa wiki hiyo ni fursa kwa jamii kuhakikisha watoto wote wanaostahili kupata chanjo wanapatiwa kwa mujibu wa ratiba, na kuzitaka huduma za afya kuendelea kuwa karibu na wananchi wote wanaohitaji chanjo.
“Kiwango hiki cha uchanjaji, pamoja na afua nyingine za kiafya, kimesaidia kupunguza vifo vya watoto chini ya miaka mitano na kufanikisha malengo ya Maendeleo Endelevu (SDG 4),” alisema.
Pia ameitaka jamii kuwa mstari wa mbele kuhakikisha watoto wanapata chanjo, akionya kuwa kutowachanja kunaweka maisha yao hatarini. SOMA: Halmashauri kufuatilia huduma za chanjo Mtwara
Katika maadhimisho hayo, chanjo ya saratani ya mlango wa kizazi kwa wasichana wa miaka tisa pia inatolewa, ambapo Mhagama ametoa wito kwa wazazi kuhakikisha mabinti wote waliokosa chanjo hiyo wanapatiwa haraka.
Ameongeza kuwa Serikali ya Rais Dk. Samia Suluhu Hassan, kwa kushirikiana na Shirika la GAVI, inaendelea kuimarisha huduma za chanjo kupitia maboresho ya mnyororo baridi wa utunzaji wa chanjo nchini.
Kwa upande wake, Mkurugenzi wa Huduma za Uuguzi na Ukunga, Ziada Sellah, akimuwakilisha Mganga Mkuu wa Serikali Dk. Grace Magembe, alisema dhima ya maadhimisho hayo ni kuwahusisha wadau mbalimbali katika kuboresha huduma za chanjo kitaifa, pamoja na kuelimisha jamii kuhusu umuhimu wa chanjo dhidi ya magonjwa kama Surua Rubella, Nimonia na Kuhara.