Mazishi ya mfamasia aliyeuawa yasubiri uchunguzi

mshumaa

MAZISHI ya mwili wa aliyekuwa mfamasia katika Hospitali ya Rufaa ya Temeke, Magdalena Kaduma yanasubiri uchunguzi wa polisi.

Mwili huo bado upo katika Hospitali ya Taifa Muhimbili-Mloganzila kwa ajili ya uchunguzi huo.

Mwenyekiti wa Mtaa wa Hondogo, Leonard Sabuni ambaye ni moja wa mashuhuda wakati wa upatikanaji wa mwili wa Magdalena alisema mwili wa marehemu bado upo hospitali wanaendelea kusubiri uchunguzi ukamilike ili wajue taratibu zinazofuata.

Advertisement

“Kuhusu taratibu za mazishi ni jambo ambalo lipo ndani ya familia wao ndio watajua mazishi yatafanyika lini, watakapopewa mwili mara baada ya uchunguzi wa kipolisi kukamilika, kwa sasa bado sijajua kuhusu taratibu nyingine,” alisema Sabuni.

Naye Ofisa Habari wa Jeshi la Polisi Kanda Maalumu ya Dar es Salaam, Allen Ponera alisema polisi wanaendelea na uchunguzi na ukikamilika itatolewa taarifa.

Ilidaiwa kuwa mwili wa Magdalena ulipatikana Ijumaa ya wiki iliyopita saa 9:00 alasiri ukiwa umefikiwa mita 15 kutoka ilipokuwa nyumba yake katika Mtaa wa Hondogo, Kata ya Kibamba, Wilaya ya Ubungo Dar es Salaam.

Awali, alidaiwa kutoonekana tangu alipoondoka nyumbani hapo Desemba 4, mwaka huu.