Mbappe arejea Ufaransa kwa matibabu

UJERUMANI – SHIRIKISHO la Soka nchini Ufaransa (FFF) limesema Kylian Mbappe amerejea kwenye kambi ya timu ya taifa na atatibiwa bila kufanyiwa upasuaji.

Taarifa hiyo imetolewa na shirikisho kwa vyombo vya habari baada ya hofu iliyojengeka kwa nyota kwamba huenda anaweza kufanyiwa upasuaji.

“Kylian Mbappe amerejea kwenye kambi ya timu ya Ufaransa na atapata matibabu bila ya kufanyiwa upasuaji,” alisema.

Taarifa hiyo ilielezea kuwa Mbappe atakuwa chini ya uangalizi wa madaktari maalumu wa timu. Kwa upande mwingine atatengenezewa kinyago kwa ajili ya michezo ijayo.

“Kinyago (maski) kitatengenezwa ili kuruhusu mchezaji huyo kurejea tena kwenye mashindano baada ya muda uliowekwa kwa matibabu kumalizika,” lilisema Shirikisho hilo.

SOMA: Wataalamu Fifa kushuhudia michezo Umisseta

Shirikisho limetoa taarifa hii kwa haraka mara baada ya kocha wa timu hiyo, Didier Deschamps kuonesha wasiwasi juu ya nyota huyo wakati akifanya mahojiano baada ya mchezo dhidi ya Austria juzi.

“Iko wazi timu ya Ufaransa bila yeye (Mbappe) haiwezi kuwa sawa ila nina imani atarejea,” alisema Deschamps. Mbappe alipata jeraha la pua katika mchezo wa juzi dhidi ya Austria wakati akigombania mpira na beki wa timu hiyo, Kevin Danso dakika ya 85.

Ushindi huo unakuwa wa 100 tangu kocha Deschamps apewe majukumu ya kukinoa kikosi hicho Julai 8, 2012.

Michuano ya Euro itaendelea leo ambapo itachezwa michezo mitatu, Ujerumani atacheza dhidi ya Hungary saa 1:00 usiku, Scotland dhidi ya Uswisi saa 4:00 usiku na Croatia dhidi ya Albania saa 10:00 jioni.

Habari Zifananazo

Back to top button