DODOMA: WAZIRI wa Uchukuzi Prof Makame Mbarawa ameziagiza mamlaka zinazosimamia mradi wa ujenzi uwanja wa ndege wa kimataifa wa Msalato, mkoani Dodoma kuhakikisha mkandarasi wa mradi huo anaongeza kasi ya kukamilisha hatua zilizobaki ili kukabiliana na mvua zinazotarajiwa kuanza kunyesha.
Prof Mbarawa ametoa maelekezo kwa Wakala wa Barabara (TANROADS) na Mamlaka ya Viwanja vya Ndege (TAA) wakati alipokagua maendeleo ya mardi huo uliopo Msalato, nje ya jiji la Dodoma iliyofanyika mnamo Januari 30, 2025.
“Ninapongeza kwa dhati hatua zilizofikiwa, nimeona sehemu ya kwanza inayohusisha ujenzi wa uwanja wa kurukia na kutua ndege unaogharimu shilingi Bilioni 165.65. Kazi inaendelea vizuri na imefikia asilimia 84 natoa rai msimamieni mkandarasi aongeze kasi hapa ili mvua zinazotarajiwa kuanza mwezi Machi mwaka huu zisimkwamishe,” amesisitiza Prof Mbarawa.
Alielekeza kuwa mkandarasi huyo asimamiwe vyema kuhakikisha kuwa uwekaji wa lami unamalizika ndani ya wiki mbili sababu mwezi wa tatu kutakuwa na mvua nyingi na huwezi kuweka rami wakati wa mvua
Aidha ameongeza kuwa kazi zitakazobaki za kufunga mifumo ya kuongozea ndege sambamba na sehemu ya pili ya ujenzi wa jengo la abiria ambao umefikia asilimia 70 ambavyo vinaweza kufanywa taratibu hata kipindi cha mvua vitakamilika mwishoni mwa mwezi Juni, 2025 ambapo uwanja utakuwa tayari kwa matumizi.
SOMA: Imani potofu yakwamisha wosia wa mirathi
Kwa mujibu wa waziri, uwanja huo utaleta tija kwa nchi na wakazi wa Dodoma na mikoa ya jirani.
Akitoa taarifa za mradi meneja Tanroads mkoa Dodoma, Zuhura Amani amesema mpaka sasa utekelezaji wa mradi unaendelea vizuri ambapo ujenzi wa uwanja umefikia asilimia 84.
Aliongeza kuwa ujenzi wa majengo yote likiwemo jengo la kushukia na kupandia abiria na jengo la kuongozea ndege vimefikia asilia 51 kwa ujumla huku akiahidi kuongeza kasi ya usimamiaji ili vikamilike kwa wakati na kwa thamani halisi ya fedha, jambo litakalowafanya wananchi waanze kujivunia maendeleo yanayoletwa na Serikali ya Awamu ya Sita inayoongozwa na Rais Samia Suluhi Hassan.