Imani potofu yakwamisha wosia wa mirathi Bukombe

IMANI potofu kwa wakazi walio wengi wa halmashauri ya wilaya ya Bukombe mkoani Geita juu ya suala la wosia imetajwa kuwa kikwazo kikubwa cha mgawo sahihi wa mirathi hali inayoibua migogoro ya kifamilia.

Viongozi wa vijiji tofauti katika kata ya Runzewe Mashariki wilayani Bukombe wamebainisha hayo wakati wa mikutano ya hadhara iliyoongozwa na timu ya Kampeni ya Msaada wa Kisheria ya Mama Samia.

Mtendaji wa kijiji cha Msonga, Andrew Bernard, amekiri changamoto ya wosia ni kubwa kwa sababu jamii nyingi wanaamini kwamba akishaandika wosia ndio atakuwa amejitabiria kifo.

Advertisement

Amesema katika kijiji cha Msonga, ni wananchi wachache sana walioandika wosia, jambo ambalo mara nyingi linasababisha vurugu kwenye familia hizo hasa baada ya mzazi wao kufariki dunia.

“Tunamshukuru sana mheshimiwa Rais Dk Samia Suluhu kwa maono yake aliyoyaona kuwafuata watanzania hawa wenye elimu duni juu ya sheria ili wapate ufahamu wa sheria”, amesema Bernard.

Mtendaji wa kijiji cha Kasozi, Makoye Mhozya amesema kiini cha tatizo hilo ni ukosefu wa elimu ya sheria lakini baada ya elimu hiyo watajua kuwa wosia ni jambo la msingi, siyo kwamba unakaribisha kifo.

“Naamini ni imani potofu na elimu ilikuwa haijawafikia na walikuwa hawana uelewa, na kusababisha migogoro mingi kujitokeza pale mzazi anapofariki hajaacha wosia kunakuwa na ugomvi kati ya ndugu”, amesema.

Mwenyekiti wa kijiji cha Msonga, Janeth Wilson amesisitiza wananchi wengi hawajui hatua na maana halisi ya wosia.

“Wananchi walikuwa hawajui suala hili kwamba wanapaswa kutoa wosia mapema kwa hiyo unakuta umauti unamkuta mtu mali zinaanza kugombaniwa na familia au baba akitangulia kufa, mama anataifishwa zile mali.

“Watu siku hizi hawalengi msiba tu, wanaangalia mali, msiba unaisha watu wamejikita zaidi kwenye mali baada ya msiba kwa sababu mzazi hakuacha wosia ya mali alizokuwa nazo”, amesema Wilson.

Wakili wa kujitegemea kutoka Chama cha Wanasheria Tanganyika (TLS), Esther Safari amesema zipo aina mbili za wosia ambazo ni wosia wa maandishi na wosia wa maneno (tamko).

Esther amesema wosia wa maandishi unaandikwa kwa kalamu za wino, au kwa kuchapwa ambapo unatakiwa uwe na mashahidi wasiopungua wawili na mmoja kati yao anatakiwa awe ndugu wa karibu.

“Katika wosia wa mdomo mashahidi wanatakiwa wawe wanne, ambao wawili kati yao ni ndugu wa karibu na wawili wanatakiwa wawe ni watu baki”, amesema.

Amesema mashahidi wote wasiwe na maslahi binafsi na mali ya kuandika wosia ambapo wosia huo utahifadhiwa ofisi ya uzazi na vifo, ofisi ya mwanasheria, benki, makanisani pamoja na misikitini.

“Mwandika wosia tunashauri ataje au aandike mali zake yeye tu, na asiandike mali ya mtu mwingine utakuwa umefanya makosa”, ameongeza;

“Kuna watu ambao wanaweza kunyimwa urithi katika wosia kwa mfano kama kuna mtu ambaye alitaka kumuua huyo mtoa wosia, au huyo mtoa wosia aliugua lakini hakuuguzwa na mnufaikaji.

“Watu wengi bado wanaogopa kuandika wosia kwa dhana potofu kwamba ukiandika wosia au ukitoa wosia utakuwa unajitabiria kifo, jambo ambalo si kweli wosia unapunguza migogoro sana”, amefafanua Wakili Esther.

Add a comment

Toa Jibu

Barua-pepe haitachapishwa. Fildi za lazima zimetiwa alama ya *